
Dar es Salaam. Prediabetes ni hali ya awali ambayo inaashiria kuna hatari ya kupata ugonjwa wa kisukari aina ya pili.
Katika kipindi hiki, kiwango cha sukari huwa juu ila sio juu kiasi cha kufanya uwe mgonjwa wa kisukari.
Prediabetes ni ishara ya onyo kuwa mwili unashindwa kudhibiti sukari kwa usahihi, na ikiwa haitadhibitiwa, inaweza kuwa na kisukari aina ya pili.
Prediabetes ni kama kengele inayokutaarifu kuwa unaweza kupata kisukari, Hali hii husababishwa na mtindo wa maisha na mazingira kwa ujumla.
Hali hii huwa haina dalili na mara nyingi unaweza kuumwa bila kujua unaumwa nini hadi wakati kipimo cha damu kinapoonyesha kiwango cha juu cha sukari.
Kuna sababu kadhaa zinazoongeza uwezekano wa prediabetes kufikia hatua ya kuwa kisukari aina ya pili, ikiwamo uzito wa juu na mafuta mabaya.
Mtu mwenye mafuta mengi mwilini hasa lehemu una uwezo mdogo wa kutumia insulin kwa ufanisi, hali inayoitwa ‘insulin resistance’. Hii ni sababu kubwa ya kufikia hatua ya kuwa na kisukari aina ya pili.
Pia kutofanya mazoezi. Ukosefu wa mazoezi huathiri uwezo wa mwili kutumia sukari na mafuta kwa nishati, hivyo kuongeza hatari ya kupanda kwa sukari mwilini.
Lishe isiyo sahihi: Ulaji wa vyakula vyenye sukari nyingi, wanga uliosindikwa, na vyakula vyenye mafuta mabaya, huongeza uwezekano wa mwili kushindwa kudhibiti sukari.
Historia ya familia inaweza kuwa moja kati ya sababu ya kupata prediabetes. Ikiwa mzazi au ndugu wa karibu ana kisukari aina ya pili, uwezekano wa kupata prediabetes ni mkubwa. Aidha, watu wenye zaidi ya miaka 45 wako kwenye hatari kubwa ya kupata prediabetes, ingawa prediabetes inaweza kuonekana pia kwa vijana, hasa wale wanaoishi katika mazingira yanayoweza kusababisha prediabetes.
Hali kama shinikizo la juu la damu, tatizo la lehemu. Haya yote huongeza uwezekano wa prediabetes.
Mbali na kisukari aina ya pili, prediabetes ni sababu ya magonjwa ya moyo na mishipa ya damu, kiharusi na macho.
Mara tu unapogundulika kuwa na prediabetes, unapaswa kufanyiwa vipimo vya moyo,vipimo vya macho,na kiwango cha lehemu mwilini, na viwango vya sukari kila mwaka mmoja hadi miwili.
Prediabetes ni kengele inayokupa taarifa kuwa unaweza kupata aina ya pili ya kisukari. Hii haimaanishi kuwa ugonjwa wa kisukari umeanza, bali inakupa nafasi ya kuchukua hatua mapema.
Kwa kudhibiti uzito, kufanya mazoezi, kuwa na tabia ya ulaji wa makundi yote ya chakula kwenye mlo mmoja, unaweza kuzuia ugonjwa wa kisukari aina ya pili, kupunguza hatari ya magonjwa ya moyo, kiharusi, na kudumisha afya.