Colonel Michael Randrianirina wearing a uniform, green beret and sunglasses

Chanzo cha picha, AFP/Getty Images

    • Author, Sammy Awami
    • Nafasi, BBC Africa
    • Author, Omega Rakotomalala
    • Nafasi, BBC Monitoring

Kanali Michael Randrianirina ameapishwa kuwa Rais mpya wa Madagascar katika Mahakama ya Katiba Kuu jijini Antananarivo.

Anamrithi Andry Rajoelina, rais wa zamani aliyeikimbia nchi na baadaye kuondolewa madarakani kufuatia maandamano ya kudai uwajibikaji zaidi.

Katika hotuba yake ya kuapishwa, Randrianirina aliahidi kutekeleza majukumu yake kwa haki na kujitolea kuilinda umoja wa kitaifa na haki za binadamu.

“Nitatekeleza kikamilifu, kwa ukamilifu na kwa haki majukumu makuu ya wadhifa wangu kama Rais wa Jamhuri ya Madagascar,” alisema Randrianirina katika hafla ya kuapishwa katika Mahakama ya Katiba Kuu.

“Ninaapa kwamba nitaitumia mamlaka niliyopewa kwa uadilifu na kujitolea kwa nguvu zangu zote kulinda na kuimarisha umoja wa kitaifa na haki za binadamu,” aliongeza.

Alitangaza kuwa jeshi limechukua madaraka, kuvunja taasisi zote isipokuwa Bunge la Taifa, na kwamba serikali ya mpito itaongoza hadi miaka miwili kabla ya uchaguzi mpya.

Haya yanajiri baada ya Umoja wa Afrika kutangaza vikwazo dhidi ya Madagscra wakieleza ukiukaji wa kikatiba.

.

Chanzo cha picha, Reuters

Rais wa Mahakama ya Katiba Florent Rakotoarisoa ameikosoa jumuiya ya kimataifa kwa kuelezea hali ya Madagascar kuwa ni mapinduzi.

Alisema kuwa hakuna ukiukwaji wa katiba nchini Madagascar, badala yake analaumu katiba kwa kusababisha hali kuwa mbaya.

Waandamanaji walikuwa na matumaini kwamba Rajoelina angejiuzulu na ili kutoa nafasi ya mabadiliko ya kidemokrasia.

Badala yake, aling’ang’ania madaraka, akiivunja serikali yake na kufanya mijadala mingi na makundi mbalimbali ya watu, juhudi ambazo hazikutosha kuwatuliza waandamanaji.

Maandamano hayo, yaliyoanza mwezi uliopita, yaliandaliwa na vuguvugu la vijana linalojulikana kama Gen Z – lililokasirishwa na ukosefu wa umeme na maji.

Kanali Randrianirina alikuwa mkuu wa kitengo cha jeshi cha Madagascar cha CAPSAT, wakati siku ya Jumanne wanajeshi wake walijiunga na maelfu ya waandamanaji kwenye mitaa ya mji mkuu.

Aliwaambia waandamanaji wa Gen Z kwamba anachukua mamlaka na kwamba jeshi litaunda serikali na kufanya uchaguzi ndani ya miaka miwili.

Watetezi wa demokrasia, ndani na nje ya nchi, wanatumai kuwa ahadi hii itatekelezwa.

Kabla ya kuapishwa kwa Ijumaa, aliongeza kuwa kufanya mageuzi katika tume ya uchaguzi na kusafisha orodha ya wapiga kura ni muhimu kabla ya uchaguzi mpya kufanyika, kulingana na tovuti ya habari ya L’Express de Madagascar.

Maelezo zaidi kuhusu Madagascar:

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *