Nairobi, Kenya. Mwili wa Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, umepelekwa katika majengo ya Bunge la Taifa jijini Nairobi leo Ijumaa, Oktoba 17, 2025.
Mwili huo umewasili bungeni ukiwa umebebwa na gari la kijeshi, katika hafla iliyoambatana na gwaride maalumu na wimbo wa Taifa, ikiwa ni sehemu ya heshima za mwisho kwa kiongozi huyo mashuhuri wa upinzani nchini humo.
Ikumbukwe kuwa awali, shughuli hiyo lilipaswa kufanyika jana, lakini likalazimika kuahirishwa kutokana na wingi wa wananchi waliojitokeza kumuaga nguli huyo wa siasa za Kenya.
Taarifa kutoka Bunge la Taifa zinaeleza kuwa wabunge wote waliombwa kufika mapema leo asubuhi kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa, wananchi wa Nairobi watapata fursa ya mwisho ya kuuaga mwili wa Raila Odinga leo Ijumaa katika Uwanja wa Nyayo kabla ya kupelekwa nyumbani kwake Bondo, Kaunti ya Siaya na mazishi rasmi ya kitaifa yatafanyika siku ya Jumapili.