Hamas imejaribu kurejesha utulivu huko Gaza, lakini imekabiliana na upinzani kutoka kwa makabila yenye silaha.

Chanzo cha picha, Getty Images

    • Author, Monitoring section
    • Nafasi, BBC

Mapatano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano Gaza yameweka wazi mapungufu katika mfumo wa usalama wa ndani, na kufichua uwepo wa vikundi vilivyojihami ambavyo vinapambana na Hamas kwa kushirikiana na Israel.

Mnamo Juni, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, alieleza kuwa serikali yake imefanikiwa “kuhamasisha baadhi ya makabila ndani ya Gaza” ili kupambana na Hamas.

Miongoni mwao ni kabila la Daghmash, ambalo lilihusishwa na mapigano yaliyosababisha kifo cha mwandishi wa habari na mwanaharakati mashuhuri wa Kipalestina, Saleh Jaafaravi.

Kwa mujibu wa ripoti mbalimbali, baadhi ya viongozi wa vikundi hivi ni maafisa wa zamani wa usalama kutoka harakati ya Fatah au Mamlaka ya Palestina.

Hamas inatuhumu magenge hayo kwa kushirikiana na mashirika ya ujasusi ya Israel, kama Yasser Abu Shabab, kiongozi wa wanamgambo wa Rafah, Hussam Astel, na Rami Halas.

Mnamo Oktoba tarehe 15, Kikosi cha Kuzuia cha Hamas kilionya upinzani katika ujumbe wa Telegraph “kusahihisha mwenendo wao” na kukipa jeshi habari muhimu kuzuia upanuzi wa kundi linalopinga Hamas.

Makundi haya yenye silaha yameongezeka wakati wa vita vya miaka miwili vya Gaza, mtaalam wa usalama aliiambia tovuti ya Lebanon ya Al-Mudoun. Tovuti ya Emirati ya Aram News pia iliripoti kwamba vyanzo vilielezea mapigano kama “vita vya kujihami kimaisha.”

Wakati huo huo, gazeti la mjini London la Asharq Al-Awsat, likinukuu chanzo “karibu na Abu Shabab,” liliandika kwamba kundi hilo hadi sasa limeajiri mamia ya wapiganaji na limewapa mishahara “mnono”.

Pia unaweza kusoma:

Je, ni vikundi gani vikuu vya wanamgambo vinavyofanya kazi katika Ukanda wa Gaza?

Hivi sasa, makundi kadhaa ya wanamgambo yanafanya kazi katika Ukanda wa Gaza, mojawapo likiwa na mafungamano na Yasser Abu Shabab na lina makao yake makuu katika mji wa kusini wa Rafah.

Kuna kundi jingine linaloitwa “Al-Qawat Al-Shaabiyyah” (Majeshi Maarufu), ambalo linasemekana kuwa na uhusiano na Abu Shabab. Inaongozwa na Ashraf al-Mansi na inafanya kazi kaskazini mwa Gaza, ikiwa ni pamoja na Beit Lahia na Jabalia.

Mnamo Oktoba 14, Mansi aliwaonya Wapalestina kaskazini mwa Gaza katika ujumbe uliorekodiwa kutokaribia maeneo yanayodhibitiwa na Hamas.

Yasser Abu Shabab hapo awali alikamatwa na Hamas kwa tuhuma za uhalifu. Inasemekana kuwa Israel ililipatia kundi lake silaha, na vyombo vya habari vimeripoti sana juu ya uwezekano wa uhusiano wake na Israel.

Ripoti ya Umoja wa Mataifa ilimtaja Abu Shabab kuwa mhusika mkuu katika uporaji mkubwa wa misaada ya kibinadamu. Inadaiwa kuwa kundi lake lina wapiganaji zaidi ya 100, huku ikiripotiwa kuwa Israel iliwapatia silaha.

Sehemu wanazofanya kazi

Kwa mujibu wa Iram News, kundi la pili la wanamgambo linaloongozwa na Rami Hales linaendesha harakati zake katika mji wa Gaza na linaundwa na makumi ya watu wa familia ya Hales, ambao baadhi yao ni wa vuguvugu la Fatah. Iram News ilielezea kundi hilo kama “kundi la wapiganaji lililopangwa zaidi katika jiji.”

Kundi la tatu lililotajwa na “Aram News” liko katika mji wa Khan Yunis na linaongozwa na Hessam Astel.

Kuna kundi jingine lenye silaha linaloongozwa na Yasser Hanidaq, linaloundwa na makumi ya wanachama wa zamani wa harakati ya Fatah. Kando yake kuna kundi la wanamgambo wenye mfungamano na kabila la Daghmash, ambalo linasemekana kuungwa mkono na jeshi la Israel.

Hossam Estal na Rami Hales ni akina nani?

Hussam Astel ni afisa wa zamani wa usalama wa Mamlaka ya Palestina ambaye anaongoza kundi la wanamgambo lenye makao yake makuu huko Khan Yunis kusini mwa Ukanda wa Gaza.

Anasemekana kuunga mkono makundi ambayo Hamas kwa sasa inayakandamiza. Ukoo wake unasemekana kumfukuza.

Rami Adnan Halas, 46, ni afisa wa Walinzi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina na mwanachama wa vuguvugu la Fatah. Alisema anaongoza kundi linaloitwa “Vikosi vya Ulinzi vya Watu” (Qawyat al-Difa’ al-Sha’bi) huko Gaza.

Mnamo Oktoba 7, aliuambia mtandao wa Kiarabu “Jasour News” kwamba “ameratibiwa kikamilifu na Mamlaka ya Palestina,” akiongeza kuwa takriban watu 500 walikuwepo katika eneo ambalo anadhibiti.

Wakati wa ukandamizaji wa Hamas, makundi haya na viongozi wao wako wapi?

Kufuatia makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano kati ya Hamas na Israel, na kuanza kwa operesheni za Hamas kukandamiza makundi yenye silaha, uvumi umeibuka kuhusu Abu Shab aliko.

Gazeti la Rai al-Youm lenye makao yake London London liliripoti kwamba, kwa kuzingatia machapisho ya mitandao ya kijamii, mawasiliano na Abu Shabab yamekatwa.

Gazeti hilo lilinukuu duru za habari zikisema: “Jeshi linalokalia kwa mabavu la Israel limemwachilia wakala wake, Abu Shabab, na kundi lake.”

Tovuti ya Al-Madin iliripoti mnamo Oktoba 14, ikimnukuu mtaalamu wa usalama, kwamba “baadhi ya makundi ya wapiganaji yapo katika maeneo yaliyo chini ya udhibiti wa vikosi vinavyovamia.”

Aliongeza kuwa kundi la wanamgambo wa Abu Shabab liko katika eneo la Al-Shuqa mashariki mwa Rafah, kundi la Hussam Astall liko kusini mwa Khan Yunis, na vikosi vya Rami Halas viko katika eneo la Al-Shuja’iya mashariki mwa Mji wa Gaza.

Al-Madon iliripoti kwamba vikundi vingine vina uhusiano na familia kadhaa maalum na hufanya kazi katika maeneo tofauti ya Ukanda wa Gaza.

Je, vikundi hivi vinashirikiana?

Kumekuwa na ripoti chache za uhusiano wa moja kwa moja kati ya makundi haya yenye silaha huko Gaza.

Mambo mawili wanayoonekana kuwa sawa ni madai yao ya kuunga mkono Israel na kuhusishwa na baadhi ya wanachama wao kwenye vuguvugu la Fatah.

Gazeti la The Times of Israel liliripoti kuwa, kulingana na taarifa zilizothibitishwa, makundi hayo mawili, Abu Shabab na Astel, yalikuwa yanawasiliana.

Vyombo vya habari vya Israel vinasemaje kuhusu makundi haya?

Shirika la utangazaji la Israel la Kan liliripoti kuwa vikosi vya usalama vya Hamas vilipambana na kundi hilo katika kitongoji cha Sabra huko Gaza mwishoni mwa juma lililopita baada ya kundi lililojihami lenye mafungamano na ukoo wa Daghmash kuanzisha operesheni iliyoitwa “Kampeni ya kulipiza kisasi.”

Tovuti ya habari ya Israel ya Ynet iliripoti tarehe 9 Oktoba kwamba kuongezeka kwa makundi yanayoungwa mkono na Israel, na washirika wake kunajiri baada ya makamanda wakuu wa Hamas kuuawa katika kipindi cha miaka miwili ya mapigano, na pia kunatokea huku kukiwa na hali ya kutoridhika miongoni mwa Wapalestina huko Gaza juu ya uharibifu mkubwa na ukosefu wa usalama.

Tovuti hiyo ilinukuu ukoo wa Abu Shabaab huko Rafah wakisema: “Tumefurahishwa na usitishwaji wa mapigano; tutajitahidi kwa Gaza isiyo na ugaidi na vita.”

Kulingana na Ynet, kama sehemu ya juhudi za Hamas za kuzuia kuenea kwa ushawishi wa koo, vuguvugu hivi karibuni lilijaribu kumuua Yasser Abu Shabab, lakini lilishindwa.

Abu Shabab alisema katika mahojiano tofauti na Ynet mnamo Oktoba 12: “Hamas ni shirika dhaifu na litaanguka mapema au baadaye.”

Ripoti hiyo ilitolewa baada ya mapigano ya silaha kati ya vikosi vya Hamas na ukoo wa Abu Warda katika bandari ya Gaza mnamo Oktoba 9, ambayo yalisababisha vifo vya takriban watu watano. Makumi ya wakimbizi wa Kipalestina pia waliripotiwa kuuawa.

Katika wiki za hivi karibuni, ripoti pia zimechapishwa za mapigano kati ya Hamas na kabila la Al-Majida katika mji wa Khan Yunis.

Hussam Astel, mkuu wa kabila la Al-Majida, aliiambia Ynet mnamo Oktoba 12 kwamba “anawasiliana moja kwa moja na nchi kadhaa za Magharibi, ikiwa ni pamoja na Marekani na hata Israeli,” na kwamba lengo lake ni “watu kuishi tena kwa amani, kama walivyofanya kabla ya Oktoba 7.”

Katika wito wake wa amani, pia alitoa wito kwa Waisraeli kusafiri hadi Gaza na kutaka kuachiliwa kwa mateka wote wa Israeli, Ynet iliripoti. “Tumegundua jinsi Hamas ilivyo dhaifu na inategemea zaidi propaganda.”

Ynet alikariri kuwa makabila haya yako chini ya ulinzi wa Israel na kwamba Israel imejaribu kuyatumia kusimamia usambazaji wa misaada ya kibinadamu na kuratibu katika baadhi ya maeneo.

Migogoro ya ndani bado ipo

Ynet, akinukuu “vyanzo vya Gaza” ambavyo havikutajwa majina, liliandika kwamba mwisho wa vita na Israel hauwezi kumaanisha mwisho wa migogoro ya ndani katika eneo hilo, na kwamba makabiliano mapya dhidi ya Hamas yataendelea.

Gazeti linalozingatia usalama la Ma’ariv liliripoti Oktoba tarehe 11 kwamba “silaha ya siri ya Israel inapata nguvu” na kwamba taasisi zake za usalama vinayaunga mkono makabila ya Gaza, sambamba na makubaliano ya hivi karibuni ya kusitisha mapigano.

Gazeti hilo liliripoti kuwa Israel inakusudia kutoa msaada na usaidizi wa kiusalama kwa makundi yenye silaha yanayopigana na Hamas, ikiwachukulia kama nguvu halali na mbadala wa Hamas. Hata hivyo, maelezo kuhusu aina na asili ya msaada huu bado hayajatangazwa wazi.

Gazeti la Ma’ariv liliandika kwamba moja ya chaguzi zinazozingatiwa ni kuhamishwa kwa idadi ya makabila yenye silaha hadi “Eneo la mstari wa njano” huko Gaza, eneo ambalo majeshi ya Israeli yapo na ambapo makabila hayo wanatarajiwa kuwekwa chini ya ulinzi wa Israel

Soma pia:

Imetafsiriwa na Mariam Mjahid na kuhaririwa na Ambia Hirsi

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *