Matayarishao ya maziko ya mwanasiasa mashuhuri wa Kenya Raila Odinga, aliyefariki dunia juzi Jumatano akiwa na umri wa miaka 80 alipokuwa anatibiwa nchini India, yanaendelea na tayari viongozi wa nchi za kigeni wameanza kuwasili mjini Nairobi kushiriki kwenye maziko hayo yanayotarajiwa kufanyika kashokutwa Jumapili jimboni kwake Bondo.

Mwili wa Odinga uliwasili Nairobi jana Alkhamisi ukisindikzwa na jeshi, jambo linalodhihirisha jinsi hadhi yake kama mwanasiasa ilivyokuwa kubwa.

Idadi kubwa ya waombolezaji walijitokeza kuonesha ushawishi wake wa miongo kadhaa kama mpigania uhuru, mfungwa wa zamani wa kisiasa na mmoja wa viongozi wakuu katika siasa za Kenya.

Jana Alkhamisi vikosi vya usalama vya Kenya vililazimika kufyatua risasi za moto na mabomu ya kutoa machozi kutawanya umati mkubwa wa watu waliokusanyika uwanjani sehemu ambayo mwili wa Odinga ulikuwa umelazwa.

Vurugu hizo zilisababisha vifo vya watu wasiopungua wanne na kuongeza hali ya mvutano ndani ya taifa hilo ambalo tayari linaomboleza kifo cha mwanasiasa huyo mashuhuri.

Raila Odinga, ambaye aliwania urais mara tano bila ya mafanikio, alikuwa kiongozi wa upinzani wa kudumu ambaye kampeni zake mara nyingi zilileta vurugu na kubadilisha muundo wa serikali.

Waziri Mkuu huyo wa zamani wa Kenya, Raila Odinga, atazikwa Jumapili karibu na babake, hayati Jaramogi Oginga kwenye eneo la Bondo, kaunti ya Siaya, na hivyo kufunga ukurasa wa maisha mapya katika historia ya Kenya bila ya kuweko mwanasiasa machachari kama Raila Odinga. Mustakbali wa chama chake cha ODM pia ni udadisi ambao watu wengi wanao hivi sasa baada ya kufariki duniani Raila.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *