Dar es Salaam. Mgombea ubunge wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Jimbo la Kibamba, Angellah Kairuki, ameeleza mafanikio kadhaa ya maendeleo yaliyotekelezwa katika jimbo hilo katika kipindi cha miaka minne, akisema ni kielelezo cha utekelezaji wa ilani ya CCM na dhamira ya Serikali kuboresha maisha ya wananchi.

Akihutubia wakazi wa Kibamba katika mkutano wa kampeni, Kairuki amesema Serikali imeendelea kuweka kipaumbele katika sekta za elimu, miundombinu na ustawi wa jamii, hatua ambayo imechangia kuimarisha huduma kwa wananchi.

“Katika kipindi cha miaka minne iliyopita, tumefanya maboresho makubwa kwenye shule zetu, ikiwemo ukarabati wa madarasa katika Shule ya Msingi Kiluvya na Shule ya Sekondari Kibamba,” ameema Kairuki.

Aidha, ametaja ujenzi wa ukuta wa uzio katika Shule ya Msingi Kibamba wenye thamani ya Sh milioni 50 kuwa ni miongoni mwa miradi iliyotekelezwa kwa lengo la kuongeza usalama wa wanafunzi.

Ameongeza kuwa CCM itaendelea kushirikiana na wananchi kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inakamilika kwa wakati na inawanufaisha moja kwa moja wakazi wa jimbo hilo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *