Azam FC imetoa wito kwa Watanzania kuchangamkia nafasi ya Mtendaji Mkuu iliyoachwa wazi na Abdulkarim Nurdin maarufu kama Popat. 

Hivi karibuni, klabu hiyo yenye maskani yake Chamazi jijini Dar, ilifanya mabadiliko ya kimfumo yaliyoathiri baadhi ya nafasi ikiwemo ya Mtendaji Mkuu Popat aliyepandishwa cheo na kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais.

Nafasi aliyoiacha bado iko wazi lakini kwa mujibu wa Thabith Zakaria, mkuu wa idara ya habari na mawasiliano ya klabu hiyo, hakuna hata Mtanzania mmoja aliyechangamkia nafasi hiyo.

“Ni kweli tumepokea CV (wasifu) nyingi sana kutoka nje ya nchi, ikiwemo majirani zetu Kenya, lakini hakuna hata Mtanzania mmoja aliyeandika barua ya kuomba kujaza nafasi hiyo,” amesema.

Thabith Zakaria maarufu kama Zaka Zakazi, amesema Bodi ya Klabu ya Azam inaendelea na tathmini ya CV ilizopokea lakini bado inaendelea kupokea hivyo kuwataka Watanzania kujaribu bahati yao.

“Kwa miaka mingi kumekuwa na swali maarufu la ‘Azam inakwama wapi’ huku watu wengi wakionesha kujua muarobaini wa Azam FC kufanikiwa.

“Sasa huu ni wakati wa kuomba kazi ili wafanye kile walichokuwa wanakisema,” amesema.

Azam FC imekaa bila kuwa na mtendaji mkuu tangu Septemba 10, 2025 ilipofanya mabadiliko haya huku Popat akiendelea kukaimu nafasi hiyo hadi atakapopatikana mrithi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *