Jeshi la Polisi mkoani Geita linamshikilia Martha Japhet (44), mkulima na mkazi wa Kitongoji cha Mzalendo, Kijiji cha Mawemeru, Kata ya Nyarugusu, Wilaya ya Geita kwa tuhuma za mauaji ya mume wake aliyefahamika kwa kwa jina la Shabani Paschal (55), mkulima na mchimbaji madini.

Tukio la mauaji limebainika Oktoba 16, 2025 katika Kitongoji cha Mzalendo, baada ya taarifa kufikishwa kituo cha polisi ikieleza kuwa Shabani Paschal hajaonekana nyumbani kwake tangu Oktoba 11, 2025. Kufuatia taarifa hiyo, Jeshi la Polisi lilianza uchunguzi na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa Martha Japhet na kumhoji kwa mujibu wa sheria.

Katika mahojiano hayo, mtuhumiwa alikiri kuhusika katika tukio hilo na kueleza kuwa, alimshambulia mume wake kwa kutumia kitu chenye ncha kali sehemu ya kichwani, baada ya kugundua kuwa amefariki, alichimba shimo ndani ya chumba walichokuwa wanalala, akamzika, akajaza kifusi cha udongo kisha kuweka magunia ya mihogo (udaga) juu yake ili kuficha ushahidi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Jeshi la Polisi baada ya uchunguzi wa awali chanzo cha tukio hilo ni migogoro ya kifamilia, hadi kufikia sasa uchunguzi unaendelea na mara baada ya kukamilika, mtuhumiwa atafikishwa mahakamani.

#AzamTVUpdates
✍ Ester Sumira
Mhariri | @claud_jm

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *