
Dar es Salaam. Hakuna ubishi kwamba aliyekuwa waziri mkuu na kiongozi wa upinzani Kenya, Raila Odinga (80) amelala na heshima yake.
Mlolongo wa matukio tangu alipoaga dunia hadi jana Rais wa Kenya, William Ruto alipoongoza waombolezaji kuaga mwili wake, hali hiyo imejinyesha dhahiri.
Hivyo, haikushangaza pale Rais Ruto alipomtangaza Raila maarufu kama Baba, kuwa si tu mwanasiasa mkongwe, bali “roho ya demokrasia ya Kenya, alama hai ya mapambano ya haki, uwajibikaji na utawala wa kikatiba.”
Akihutubia maelfu ya waombolezaji waliokusanyika katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi leo Oktoba 17, 2025, Ruto amesema Kenya itaendelea kuenzi urithi wa kisiasa na kimaadili ulioachwa na Raila Odinga.
“Baba Agwambo, umekuwa roho ya demokrasia yetu kupitia dhoruba na usaliti wa jela, lakini ulikuwa mwaminifu kwa wito wa juu zaidi wa kuwa mzalendo wa Kenya,” amesema Rais Ruto.
Katika tukio hilo lililojumuisha viongozi kutoka mataifa mbalimbali, miongoni mwa wageni wa heshima, walikuwepo Makamu wa Rais wa Tanzania, Dk Philip Mpango; Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mahamoud Thabit Kombo na Rais mstaafu wa Awamu ya Nne wa Tanzania, Jakaya Kikwete.
Ruto ameahidi kuwa yeye na Serikali yake wataendeleza makubaliano aliyokuwa nayo na Raila kuhusu mustakabali wa Taifa hilo, akisema urithi wa Odinga hautafutika katika historia ya Kenya wala Afrika.
Katika hatua nyingine, Ruto amemsifu Odinga kwa namna alivyoshikilia misingi ya haki, usawa na umoja wa kitaifa, akisisitiza kuwa Serikali yake itabaki kuwa mwaminifu kwa maono na juhudi ambazo kiongozi huyo alianzisha.
Kenya haitarudi nyuma
Awali, akiwasilisha salamu zake, Rais mstaafu wa Kenya, Uhuru Kenyatta alimtaja Raila kama mtu aliyechagua kuweka mbele masilahi ya Taifa, badala ya siasa binafsi au za kikabila.
“Raila alipenda nchi yake kuliko kitu kingine chochote. Hakuwa na ukabila. Alipenda Kenya yote na wananchi wake wote,” amesema Kenyatta, akiongeza kuwa nyumbani kwa Raila kulijaa marafiki kutoka kila pembe ya Kenya.
Akizungumzia mchango wa Raila katika Taifa hilo, Uhuru amesema historia ya demokrasia ya Kenya kamwe haiwezi kuandikwa bila kumtaja kutokana na namna alivyojitoa, huku akiweka masilahi ya Taifa mbele.
“Historia ya demokrasia ya Kenya haiwezi kuandikwa bila jina la Raila Odinga likiwa namba moja. Historia ya haki za binadamu, ugatuzi na nguvu za wananchi mashinani haiwezi kujadiliwa bila kumtaja Raila Amolo Odinga,” amesema.
Kwa mujibu wa Uhuru, Raila alikuwa wa kupigiwa mfano si tu kwa wanasiasa, bali kwa wananchi wote wanaopigania haki.
“Tunapomuaga leo, tujiapize kama Wakenya kwamba hatutaruhusu haki za binadamu, demokrasia na maadili aliyoyasimamia Raila yarudi nyuma,” amesema.
Alifariki akiwa imara
Winnie Odinga, binti wa marehemu Odinga amesimulia tukio la kifo cha baba yake akieleza alikuwa naye hadi pumzi ya mwisho, alipofariki dunia akipatiwa matibabu nchini India.
“Nilikuwa India wakati baba alipofariki. Alifia mikononi mwangu, lakini hakufa kama watu wanavyoeleza kwenye mitandao ya kijamii. Baba alikuwa na afya njema,” amesema.
Amefichua kuwa, Raila alikuwa na ratiba ya mazoezi ya kila siku hadi siku chache kabla ya kifo chake.
“Siku ya kwanza alitembea raundi moja, siku ya pili raundi mbili, siku ya tatu raundi tano. Aliendelea hivyo. Baba amefariki dunia akiwa mwenye nguvu na afya. Mfalme amelala, lakini urithi wake utaishi milele,” amesema Winnie, mtoto wa mwisho wa Odinga.
Winnie amemkumbuka baba yake kama mtu wa hekima, mwenye upendo kwa familia na hasa kwa wajukuu wake.
“Alikuwa baba aliyejitoa kwa familia. Hata akiwa na majukumu mengi, hakusahau wajukuu zake; alituma ujumbe wa upendo kila mara,” amesema na kuongeza:
“Sijui nitamkosa nani zaidi, baba yangu au shujaa wangu. Mimi ndiye msichana mwenye bahati kwa sababu ulikuwa baba yangu.”
Alichukia rushwa
Ida Odinga, mjane wa Raila amesema alikuwa mumewe na msimamo usiobadilika dhidi ya tamaa, unafiki na rushwa.
“Raila alichukia unafiki, alichukia tamaa ile tamaa iliyoharibu misingi ya maadili katika jamii. Hakupenda kuona watu wanaiba mali ya umma au kutumia madaraka vibaya,” amesema.
Amezungumzia miaka 52 ya ndoa yake na Odinga, akielezea jinsi walivyokutana mwanzoni mwa miaka ya 1970, wakapendana na hatimaye kufunga ndoa mwaka 1973.
Amesema ndoa yao ilistahimili mitihani mikubwa, hasa wakati Raila alipokuwa mfungwa wa kisiasa kwa sababu ya uasi dhidi ya Serikali ya wakati huo.
“Safari yetu ya ndoa haikuwa rahisi. Tulikumbana na pandashuka nyingi, lakini kadiri tulivyoendelea kuishi pamoja, tulijifunza jinsi ya kukabiliana na changamoto zilizojitokeza. Tulijifunza kuzungumza kwa uwazi, kusema ukweli, kusamehe na kusonga mbele,” amesema.
Ameeleza jinsi Raila alivyolipenda Taifa lake kwa dhati, akitoa wito kwa Wakenya kudumisha amani kwa heshima ya mume wake.
“Raila alichukizwa sana na watu waliofuja mali ya umma na wale wanaojipatia mali kwa njia za kifisadi,” amesema.
Amewashukuru Wakenya kwa mshikamano na namna walivyojitokeza kwa wingi kuomboleza pamoja nao.
“Kwa upendo wenu, maombi na mshikamano mliouonyesha tangu kutangazwa kwa kifo cha Raila, familia yetu imefarijika,” amesema.
Hali ilivyokuwa
Awali, baada ya mwili kuwasili kwenye Uwanja wa Nyayo, gari maalumu lililobeba mwili wa Odinga lilizunguka uwanja huo mara tatu kama ishara ya kutoa heshima kwa kiongozi huyo.
Tofauti na jana, Oktoba 16, ambapo kulitokea kadhia nyingi katika Uwanja wa Kasarani, leo Oktoba 17 hali ilikuwa tofauti, kwani wananchi wengi walimuaga mpendwa wao kwa utulivu huku ulinzi ukiwa umeimarishwa.
Huzuni ilitawala uwanja hapo, huku magari ya kijeshi yakifanya mizunguko kutoa heshima na watu wakibeba matawi na kupunga mikono kwa ishara ya kumuaga “Baba”.
Wakati shughuli hiyo ikiendelea, usalama uliimarishwa kufuatia vurugu zilizotokea awali, ambapo watu watatu walipoteza maisha baada ya kukanyagwa na wengine kufariki wakati polisi walipofyatua mabomu ya machozi kudhibiti umati.
Waombolezaji wameketi kwa utulivu, wakisikiliza hotuba mbalimbali za kumbukumbu kutoka kwa viongozi walioguswa na maisha ya Odinga.
Shughuli hiyo pia ilihudhuriwa na viongozi kutoka mataifa mbalimbali, wakiwemo marais, mawaziri wakuu wastaafu, wajumbe kutoka Umoja wa Afrika (AU) na viongozi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Odinga aliwahi kuhudumu kama Mjumbe Maalumu wa AU wa miundombinu na alihusishwa na jitihada mbalimbali za kuleta amani na maendeleo barani Afrika.
Katika salamu zao, viongozi hao walimwelezea kama mtetezi wa haki barani Afrika na mpatanishi wa watu na mataifa.
Alikuwa nguzo ya mazungumzo ya kisiasa na alihamasisha utatuzi wa migogoro kupitia njia za kidiplomasia.
Kuzikwa Bondo
Kwa mujibu wa wasia wake, Odinga alitaka azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake, hivyo mazishi yanatarajiwa kufanyika Jumapili, Oktoba 19, 2025, katika Kijiji cha Kang’o Ka Jaramogi, eneo la Bondo, Kaunti ya Siaya.
Maandalizi yamekamilika na Serikali imesema shughuli hiyo itakuwa ya heshima za kitaifa, huku wananchi wakipewa nafasi ya mwisho ya kuuaga mwili wake kabla ya maziko.
Sauti ya wapinzani
Raila Odinga alikuwa kiongozi wa pekee ambaye aligombea urais mara tano bila kushinda, lakini alibaki kuwa sauti ya upinzani na mwanamageuzi asiyechoka. Aliongoza harakati za kurejesha mfumo wa vyama vingi, alitetea Katiba mpya ya mwaka 2010 na alijenga upinzani wa kikatiba uliosaidia kubadilisha mwelekeo wa siasa za Kenya.
Aliwahi kufungwa jela kwa miaka kadhaa kutokana na msimamo wake wa kisiasa, lakini hakuwahi kukata tamaa. Aliheshimika ndani na nje ya nchi hiyo kama mtu aliyejitolea kwa ajili ya nchi kuliko masilahi binafsi.
Serikali kumuenzi
Serikali imetangaza kuwa barabara kuu moja itapewa jina la Raila Odinga, sambamba na kuanzishwa kwa kumbukumbu ya kitaifa katika Jiji la Nairobi.
Vyuo vikuu vinapanga kuanzisha masomo au vitengo vya uongozi wa kidemokrasia vikihusiana na maisha na falsafa za kisiasa za Raila.
Kwa wengi, Odinga alikuwa zaidi ya mwanasiasa. Alikuwa mwalimu wa siasa, mzalendo wa kweli na mtu ambaye alitumia maisha yake yote kutetea wanyonge.