Dar es Salaam. Wajasiriamali 20 kutoka Tanzania wameondoka kwenda nchini China kujifunza teknolojia za uzalishaji bidhaa, kununua mashine za uzalishaji sambamba na kujifunza ujuzi mpya kwenye sekta hiyo.
Wakizungumza uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere wakati wakijiandaa kuondoka wajasiriamali hao wamesema dhumuni ni kupanua wigo wa uzalishaji bidhaa zao ambapo wakirudi wataitumia fursa hiyo kuajiri na Watanzania wengine.
Safari hiyo ya wiki mbili imeratibiwa na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), ikiwa imedhamimiwa na Benki ya Equity Tanzania.
Mbali na kujifunza teknolojia mpya watatembelea viwanda, watajifunza namna ya kuagiza bidhaa pamoja na kutafuta fursa ya soko kwa kukutana na wajasiriamali wenzao wa China.
Dinasala Sami mjasiriamali kutoka Mwanza anayesindika unga wa lishe, korosho, mbegu za maboga na unga wake anayeuza bidhaa hizo hadi nje za nchi amesema anatarajia kujifunza zaidi katika safari yake hiyo.
“Kuna mafunzo naenda kujifunza, pia katika maonesho ya wajasiriamali nchini China, nitanunua na mashine pamoja na vifungashio vya bidhaa nikirudi nitaongeza wafanyakazi katika uzalishaji wangu,” amesema.
Lucy Luhasha mtengenezaji wa maua na vifungashio vya zawadi kutoka Mwanza amesema atakwenda katika viwanda vya vifungashio vya zawadi ili akirudi aanzishe kiwanda kitakachoajiri vijana na kikuza uchumi.
“Kwasasa ninavijana watatu wanaofanya kazi ya upambaji lakini nikirudi baada ya kupata mashine na ujuzi nitaajiri vijana wengi zaidi,” amesema.
Mjasiriamali Doroth Kimati amesema atanunua mashine za kuchakata klipsi, mashine ya kukaanga karanga na kumenya viazi anatumia fursa hiyo kujiongezea maarifa ya uzalishaji bidhaa zake.

“NikIrudi nitaajiri vijana wasio na kazi katika uzalishaji wa bidhaa zangu hizi za chakula ili wapate kipato,” amesema.
Katibu wa TWCC mkoa wa Mwanza, Jenny Ndeto amesema safari hiyo ya mafanikio inaenda kuleta fursa mpya ya mafanikio huku akiwataka wanawake ziaid kuchangamkia fursa.
“Naenda kujifunza elimu ya ujasiriamali ili nikirudi nisiwe Jenny huyu ninayeenda. Kwenye maonesho yanayoendelea huko China tutajifunza vitu vingi zaidi,” amesema.
Akizungumzia kwa undani safari hiyo, Meneja wa Kitengo cha Wanawake na Vijana kutoka Benki ya Equity, Jackline Temu amesema kutokana na changamoto inayowakabili wanawake ikiwemo kuachwa na huduma za kibenki kama mikopo wao wamekuja na suluhisho kulisaidia kundi hilo.
“Tumekuwa mstari wa mbele kuwafikia wanawake kwa kuwapatia elimu ya fedha, kuwafikia wanawake kihuduma ndio maana mwaka jana tukaja na dirisha la Mwanamke Plus.
“Tunawasaidia kukuza biashara zao, kuwapa miongozo wote wakubwa kwa wadogo, tunahakikisha biashara zao zinakua na wanakuwa kiuchumi na kwenda hadi nje ya mipaka ya Tanzania,” amesema.
Amesema safari hiyo itawawezesha wanawake hao kujifunza upatikanaji bidhaa, watembelee viwanda, wajifunze teknolojia na fursa mbalimbali