Leo ni Jumamosi 25 Mfunguo Saba Rabiuthani 1447 Hijria Qamaria mwafaka na 18 Oktoba 2025 Miladia.

Miaka 1159 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Thabit bin Qurrah Swabi, mtaalamu wa hisabati, nyota na tabibu katika kipindi cha utawala wa Bani Abbas. Alizaliwa mwaka 221 Hijria mjini Harran uliopo eneo la Mesopotamia nchini Iraq. Thabit bin Qurrah Swabi alikuwa akizungumza lugha za Kigiriki, Kisiriyan na Kiarabu. Alisafiri kwenda mjini Baghdad, Iraq kwa lengo la kusoma na kwa usimamizi wa Muhammad bin Mussa aliyekuwa mtaalamu mkubwa Mwislamu wa hisabati na nyota kipindi hicho, Thabit bin Qurrah Swabi akaingia katika uwanja wa elimu hizo. Alibuni nadharia mpya katika uwanja wa hisabati. Aidha katika utaalamu wa nyota yeye ni katika watu wa kwanza kurekebisha chombo cha Ptolemaic. Thabit bin Qurrah Swabi aliandika vitabu vingi katika uwanja wa tiba, hisabati na nyota, vilivyofasiriwa kutoka lugha ya Kigiriki kwenda Kiarabu. Miongoni mwa vitabu hivyo ni pamoja na kile kiitwacho “Adh Dhakhiratu fii Ilmi al Twib” na “Kitabul Mafrudhaat.” 

Siku kama ya leo miaka 1078 iliyopita alizaliwa mjini (Corduba, Qurtuba) Uhispania, faqihi, mtaalamu wa hadithi, fasihi na mwanahistoria Abu Omar Yusuf bin Abdallah mashuhuri kwa jina la Abdul Birr. Alipata masomo ya msingi kutoka kwa baba yake na walimu wengine wakubwa wa kipindi hicho. Ibnu Abdul Birr aliupa umuhimu mkubwa utafiti, ambapo kwa kipindi cha muda mfupi alikuwa mmoja wa wasomi wakubwa wa mjini Andalusia. Kufuatia kukosekana amani na usalama katika mji wa Corduba, Ibn Abdul Birr alilazimika kuhamia mji mwingine wa Daynah ambao kipindi hicho ulikuwa moja ya vituo muhimu vya elimu vya Andalusia, na huko alifanikiwa kuandika vitabu vyake. Miongoni mwa athari za msomi huyu mashuhuri ni kitabu cha “al Istiiab” ambacho kinahusu maisha ya masahaba wa Mtukufu Mtume Muhammad (saw). 

Katika sikuu kama ya leo miaka 158 iliyopita, ardhi ya Alaska ilidhibitiwa na Marekani. Alaska ni ardhi yenye upana wa karibu kilometa mraba milioni moja na laki tano, huko kaskazini magharibi mwa Amerika, ambapo hii leo ni moja ya majimbo ya nchi hiyo. Hadi mwaka 1867, Alaska ilikuwa ikidhibitiwa na Russia, hata hivyo katika kipindi hicho mfalme wa wakati huo wa Urusi ya zamani hakutilia maanani umuhimu wa ardhi hiyo na hivyo mwezi Oktoba mwaka 1867  akaamua kuiuza kwa Marekani. Ni vyema ifahamike kuwa, hii leo Alaska inahesabika kuwa moja ya majimbo tajiri sana ya Marekani ambapo mwaka 1960 kulivumbuliwa mafuta na kuanza kuchimbwa katika eneo hilo hadi leo.  

Siku kama ya leo miaka 154 iliyopita alifariki dunia msomi wa Uingereza na mvumbuzi wa mashine ya kikokoteo (Calculator) kwa jina la Charles Babbage. Mwaka 1812 Miladia, Babbage aliasisi taasisi ya uchunguzi kwa ajili ya kuendeleza elimu ya hisabati na akiwa na umri wa miaka 24 akateuliwa kujiunga na taasisi ya ufalme ya Uingereza. Ni baada ya hapo ndipo akaanzisha harakati ndefu za utafiti wa kuunda mashine hiyo ya hesabu ambapo hadi kufikia mwaka 1833 Miladia akafanikiwa kuvumbua chombo hicho ambacho kilikuja kuwa mashuhuri kwa jina la Babbage. Baada ya hapo karne moja baadaye wasomi mbalimbali waliifanyia marekebisho muhimu mashine hiyo sanjari na kuifanya itumie nishati ya umeme. Ni kwa ajili hiyo ndio maana Charles Babbage akatambuliwa kwa jina la baba wa kikokoteo (Calculator). 

Charles Babbage

Miaka 103 iliyopita katika siku kama ya leo, Redio ya BBC iliasisiwa huko Uingereza. Redio ya BBC awali ilikuwa ya mtu binafasi, lakini mwaka 1927 redio hiyo iliwekwa chini ya usimamizi wa serikali na ikamilikiwa na serikali ya London. Bajeti ya redio za BBC ambazo zinatangaza kwa lugha mbalimbali za dunia inadhaminiwa na serikali ya Uingereza. Licha ya kuwa BBC inadai kwamba haipendelei upande wowote katika matangazo yake, lakini katika kipindi cha nusu karne ya hivi karibuni, chombo hicho cha kupasha habari kimegeuka na kuwa wenzo wa propaganda wa serikali ya Uingereza na hivyo kuiandalia London uwanja wa kuingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine. 

Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, msomi aliyegundua umeme, Thomas Edison, alifariki dunia. Edison alizaliwa mwaka 1847 huko Marekani. Thomas Edison hakuwa na taalumu yoyote kutoka chuo kikuu bali ni tafiti na majaribio yake mengi ndiyo yaliyopandisha juu kiwango chake cha elimu na maarifa. Akiwa kijana, Edison aliasisi maabara ya masuala ya kemia na kufanya majaribio makubwa katika maabara hiyo. Bidii ya msomi huyo ilimuwezesha kuvumbua mambo mengi ambapo muhimu kati ya hayo ni hatua yake ya kuvumbua umeme, kutengeneza lampu na gramafoni au santuri.

Thomas Edison

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *