.

Chanzo cha picha, Reuters

    • Author, Asha
    • Nafasi, BBC Nairobi

Aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya Raila Amollo Odinga nchini Kenya alifariki dunia akiwa anapata matibabu nchini India. Kifo chake kimeacha Wakenya wakiwa na huzuni.

Raila sio jina dogo, hakika linatambulika ulimwenguni kote na kama ingekuwa ni kupima siasa kwa mizani, basi uzoefu wake ungemuweka katika ngazi ya kimataifa.

Ni mwanasiasa ambaye amefanikiwa kupita mawimbi mengi ya kisiasa na uzoefu wake unamuelezea kuwa mwanasiasa shupavu.

Lakini hakuna mwanasiasa tajika asiye na utani au asiyetaniwa ama kutokana na maneno yake au jinsi anavyoendesha siasa zake.

Na miongoni mwa yale ambayo Raila Odinga alikutana nayo katika safari yake ya siasa ni pamoja na kupewa majina ya majazi au majina ya utani.

Katika makala hii, tunamkumbuka Raila Amollo Odinga na majina ya utani aliyopewa na wafuasi wake labda pengine ilikuwa ni kutokana na uzoefu wake kwenye nyanja hii.

Baba

.

Chanzo cha picha, Reuters

Baba, jina maarufu nchini Kenya ambalo Raila Odinga amehusishwa nalo kutokana na historia yake ndefu kwenye siasa.

Katika familia, ‘Baba’ ni mtu ambaye huchukuliwa kuwa kiongozi na hili ni jina ambalo limejitokeza kuonyesha ishara ya wafuasi wa Raila kwa jinsi wanavyompenda na kumuamini kama mzazi anayewaongoza vyema.

Na ndivyo wengi wanavyomchukulia Raila Odinga, kama baba yao hasa katika siasa aliyejinyima mengi kwa ajili ya demokrasia Kenya.

Baba ni jina ambalo Raila Odinga alianza kuitwa na wafuasi wake kuonyesha heshima walionayo kwake na vile wanavyofurahishwa na harakati zake za kuhakikisha Kenya inakuwa huru.

Raia wa Kenya wanamtambua Raila kama ‘Baba’ kwa mengine aliyochangia nchini Kenya kama vile mabadiliko ya Katiba ambapo alikuwa na jukumu muhimu hadi upatikanaji wa Katiba mpya mwaka 2010, ambayo ilikuwa chanzo cha uhamishaji mamlaka kutoka kwa serikali kuu hadi kwa serikali za ugatuzi.

Jina ‘Baba’ lilipata umaarufu mkubwa mnamo mwaka 2014 wakati Raila alipokuwa katika ziara yake nchini Marekani kwa muda wa takriban miezi mitatu.

Alipokuwa anarejea, wafuasi wake walikuwa mitandaoni kumfahamisha kile kilichofanyika nchini Kenya wakati hayupo.

Mitandaoni maneno yao yote yalikuwa yanaanza na “baba while you were away” wakiashiria kwamba wanahitaji Raila Odinga awasikilize.

Mwaka 2008 wakati wa uchaguzi wa urais, alikaribiana na mshindi na kuteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa pili wa Kenya katika serikali ya umoja chini ya makubaliano ya kugawana mamlaka na Rais Mwai Kibaki.

Baba ni jina ambalo kwa Raila lina uzito wa upendo wa mtoto kwa mzazi kutokana na muongozo anaompatia.

Agwambo

.

Chanzo cha picha, AFP/GETTY

Agwambo ni jina la kabila la luo linalomaanisha mtu asiyetabirika au mwenye usiri mkubwa.

Wafuasi wake walimpa jina hilo kulingana na jinsi ambavyo alikuwa akiendesha siasa zake.

Kwa wanaomjua, watakumbumba vile ambavyo alikuwa akipinga serikali waziwazi, na sio kwamba anaishia hapo, bali wakati mwingine alifika hadi kiwango cha kuandaa maandamano na kushiriki nao kiasi cha hata kutembea na wafuasi wake barabarani wakipitisha ujumbe wao.

Mbinu hii ya ushirikiano wa karibu na wafuasi wake licha ya umri wake ulifanya waliompinga au wasiomuunga mkono wakiwa na wakati mgumu.

Kwa jinsi Raila alivyokuwa katika siasa, ni mtu ambaye kama hamukuendana kisiasa, haingekuwa rahisi kupuuza uwepo wake.

Wenyewe wa siku hizi wanasema, nyota yake iling’aa ama upende au usipende.

Agwambo ni jina ambalo hutumika sana katika eneo la Nyanza ambapo Raila Odinga anatokea na mwenye ushawishi mkubwa kisiasa.

Kutokana na ushawi na wingi wa wafuasi wake wale wanaotaka kuwania viti tofauti vya kisiasa katika eneo hilo, hutafuta baraka zake na kuungwa mkono naye ili wafanikiwe.

Jakom

Jakom ni jina la luo linalomaanisha mtu ambaye ana wadhifa wa mwenyekiti, kiongozi wa kikundi fulani au mtu aliye na wadhifa wa juu na wenye mamlaka.

Jamii ya Waluo hutumia jina hilo kumtambua Raila kama kiongozi wa kabila hilo.

Na pia hii inamaanisha Raila ndio mwenye kupanga mikakati na kufanya maamuzi. Na hivi ndivyo wafuasi wake wanavyotambua uongozi wake usioyumba hasa katika siasa.

Hili limeshuhudiwa na wafuasi wake, kwani alilosema, walilifuata kwa kuamini na uaminifu mkubwa hadi atakapotoa maelekezo mengine.

.

Rao

‘RAO’ ni ufupisho wa jina lake Raila. Jina hilo limetumika kwa muda mrefu kwenye nyanja ya siasa kumtambua kiongozi huyo wa upinzani.

Na mara nyingi limekuwa likitumiwa na vijana na hasa kwenye mitandao ya kijamii.

Rais wa Wananchi

.

Chanzo cha picha, AFP

Jina hili lilikuwa maarufu baada ya Raila Odinga kula kiapo chenye utata katika bustani ya Uhuru jijini Nairobi kuwa rais wa wananchi.

Hayo yalijiri baada ya uchaguzi mkuu wa urais wa mwaka wa 2017 kukumbwa na utata.

Wakili aliyejitangaza kuwa kiongozi wa vuguvugu la National Resistance Movement (NRM) Miguna Miguna ndiye aliyemuapisha.

Mwanasiasa mashuhuri wakati huo ambaye sasa hivi ni marehemu Otieno Kajwang’ ni baadhi ya viongozi waliokuwepo.

Mzee wa Vitendawili

Raila alijipatia jina la “Mzee wa Vitendawili” kwa sababu ya kutumia vitendawili sana wakati wa kampeni za uchaguzi.

Ni jina ambalo lilitumika na wakosoaji wake wakati huo hasa Rais William Ruto kipindi akiwa Naibu Rais na mgombea uchaguzi wa chama cha United Democratic Alliance (UDA).

Miaka ya nyuma kuna wakati alihojiwa na moja ya televisheni za eneo kuhusu vitendawili vyake akiulizwa kama huwa anaviandaa kabla ya mikutano yake.

“Vitendawili huwa vinakuja vyenyewe, wakati ninakua nilikuwa nikisikiliza wakubwa zangu, na ninajua kuwa katika tamaduni za Kiafrika watu walikuwa wanazungumza kwa mafumbo, hii ni njia moja ya kuwasilisha ujumbe…,” Raila Odinga alisema.

Ingawa Raila Odinga amefariki dunia, vitendawili vyake hasa wakati anakosoa wapinzani wake vitakumbukwa milele.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *