
Benki ya Ufaransa BNP Paribas imepatikana na hatia siku ya Ijumaa, Oktoba 17, kwa kuhusika katika dhulma nchini Sudan chini ya utawala wa rais zamani Omar Al Bashir. Benki kubwa ya Ufaransa imepatikana na hatia ya kufanya kazi nchini humo na hivyo kushiriki katika ufadhili wa jeshi la Sudan na wanamgambo wenye uhusiano na utawala huo. Kesi hiyo ilifanyika New York, ambapo walalamikaji watatu wa Sudan, waliopewa uraia wa Marekani walitunukiwa karibu dola milioni 21 kama fidia.
Imechapishwa:
Dakika 1 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Ubakaji, utesaji, kukatwa kwa visu, kuchomwa kwa sigara… Walalamikaji watatu, wanaume wawili na mwanamke mmoja, walisimulia baraza la mahakama dhuluma walizopata kutoka kwa waandamizi wa serikali ya Sudan, ambao waliiba au kuharibu mali zao. Kulingana na ushuhuda wao, watu waliowafanyia dhulma hizo ni kutoka jeshi la Rais wa zamani Omar Al Bashir, madarakani kuanzia mwaka 1989 hadi mwaka 2019, au wanamgambo wa Janjaweed ambao walikuwa wakiendesha ugaidi huko Darfur.
Walalamikaji walishutumu BNP Paribas kwa kushiriki katika ufadhili wa ukandamizaji na kwa hivyo kushiriki dhulma hizo. Benki hiyo “iliunga mkono utakaso wa kikabila na kudhoofisha uwepo” wa walalamikaji, wakili wao alisema.
BNP Paribas ambayo iliendesha harakati zake nchini Sudan kuanzia mwishoni mwa miaka ya 1990 hadi 2009, iliipatia Khartoum mikopo kwa mikataba ya kibiashara ya mafuta na bidhaa za kilimo, ktoa dhamana ikiwa kutakosekana malipo.
Wanasheria wanadai benki hiyo haikuwajibika moja kwa moja
Mawakili wake walidai kuwa benki hiyo haikuwa na jukumu la moja kwa moja, na kwamba Sudan imekuwa na ghasia za mara kwa mara tangu uhuru wake, na kwamba dhuluma hizo zingetokea bila kujali uwepo wake.
Utetezi huu haukuweza kushawishi majaji, ambao waliamuru benki kuwalipa walalamikaji watatu jumla ya dola milioni 20.75 kwa uharibifu.