Dar es Salaam. Juzi mmeshuhudia kinababa na kinamama wa Ukraine wanacheza kwa furaha baada ya makubaliano ya kusitishwa kwa vita inayowasulubu. Furaha ile ni kama ya machale, bado hawajawa na uhakika kwa asilimia zote kwamba vita itaisha. 

Kama dansi la “urafiki wa mashaka” lilivyokuwa likionekana. Lakini kwa kuwa wababe wawili Marekani na Urusi wamekubaliana hivyo, basi angalau hofu itapungua. Watu watarudi kuanza ukarabati wa makazi yao, na wafanyakazi na wakulima wataendelea na shughuli zao.

Nasema mchezo ni wa machale kwa sababu kuachwa kwa vita kunaweza kupelekea wababe hao wapoteze maslahi yao ya jumla. Ukraine ni wazalishaji wakubwa wa mazao ya chakula na biashara, na tangu mwanzo tuliona vita hiyo ikihusisha uchumi zaidi ya uhasama. 

Mataifa makubwa yalipata maslahi mazuri kwenye mahusiano na nchi hiyo. Lakini wezi wawili wakiwa wanaiba kwenye mfuko mmoja, mambo hayawezi kuwa shwari baina yao.
Risasi, magruneti na hadi mabomu mazito yalirindima usiku na mchana. 

Mpaka ulifikia wakati watu walishangaa siku ilipopita kimya bila mirindimo ya mabomu. Walipokuwa kwenye shughuli za kawaida na mabomu yakasikika mtaa wa sita, waliulizana: 
“Hawa wajinga wanaanza saa hizi?” Shughuli zilisimamishwa pale mirindimo iliposogea hadi mtaa wa pili. Hapo muungwana angewasogeza watoto nyumbani, wakasubiri nyumba ibomolewe.

Mimi nakumbuka mtaani kwetu aliishi mzee aliyekuwa hajambo kidogo, na alijaaliwa mabinti warembo. Alibuni njia ya kuwapa taarifa wakware na vibaka kuwa hapo hapaingiliki. 

Hivyo kila asubuhi ya siku ya mapumziko ya mwisho wa juma, aliketi ngazini kuliosha gobore lake. Wenyeji na wageni tulikusanyika hapo kwa wingi kushuhudia mashine “Tantalila Mlango wa Chuma” ikifanyiwa usafi.

Alipomaliza alilijaribu kwa kuwatungua kunguru wezi wa kuku. Akahesabu: “Moja… mbili… ta…” Ulitoka mshindo mkubwa kila mmoja wetu alichanganyikiwa. Mwanzoni kila tuliposikia kishindo cha gobore, tulichanganyikiwa na kutoka mbio. 

Baadaye tulizoea. Kama ujuavyo akili za watoto, tulijiuliza ni namna gani lile dude lilifanya kazi. Sasa tuliwagombania kunguru waliodondoshwa na kuwakagua, hata hivyo hatukuwahi kuona kitu zaidi ya majeraha.

Ukaja wakati wa vita ya Kagera. Uwanja wa Shule tuliyosoma ulitumika kwa mazoezi ya ndege za kivita zilizoitwa Mig.21. Mwanzoni tulikuwa tukiogopa sana kwani ndege zile zilitoa moto kabla ya moshi. Lakini kadiri muda ulivyoenda tulizoea.

Tukawa tukijichagulia kila mmoja na ndege yake ya kuishangilia kwa jinsi ilivyocheza sarakasi kule angani. Lakini siku moja zilikuja tatu kama zinaanguka, halafu zikainuka kwa pamoja mbele ya nyuso zetu.

Ilikuwa nusura tupoteze fahamu. Baadaye tulimcheka mwenzetu aliyeshika shavu na kudai “mimi imenigonga hapa”.

Hakujua kuwa kwenye hekaheka zile aligongana uso na mwenzake. Mara nyingi wakati wa tukio watu watapoteza fahamu, zikija kuwarudia ndipo mama anapogundua kuwa aliopoa sufuria badala ya mtoto, mwingine atagundua kuwa ameacha miguu! Tangu siku hiyo tulikoma kucheza na ndege zile, na nakumbuka shule ilifungwa kwa muda.

Ukweli unabaki kuwa vita vya hadithi unaweza kuvizoea mara moja, lakini vita halisi ni zaidi ya majanga. Vita ni mzimu ambao kila upitapo huacha masaibu makubwa. Kwanza haina macho wala huruma, ukijipendekeza tu inakula kwako. Shughuli zote za kiuchumi na za kijamii husimama kuipisha vita hiyo.

Wewe ni nani unayeweza kukatiza kati ya mzimu wa aina hiyo, upite katikati ya mishindo ya risasi na magruneti ati unawahi kwenye vikoba!

Ni bora tunavyowasikia wadau mbalimbali wakiwemo wanasiasa, viongozi wa imani na wanajamii kwa ujumla wakitahadharisha kuhusu madhara ya vita. Ni muhimu kila mmoja atimize wajibu wake, hasa wakati huu tukielekea kwenye tukio kubwa la kidemokrasia. 

Panapofuka moshi huwa kuna moto, na moto huanza na njiti moja lakini huweza kuteketeza misitu kwa muda mfupi sana. Tutahadhari mno na kasoro ndogondogo katika uchaguzi zisije zikapeleka mikondo itakayochafua hali ya hewa.

Yapo maeneo ambayo yamezoea vita na kudhani huo ndio mpango wa Muumba wao. Kuna jamaa alituambia kwamba yeye aliwahi kupita Mashariki ya Kati katika moja ya safari zake. Anasema mahasimu waishio jirani na Hekalu Kuu huchapana risasi hadi muda wa kuswali. 
Wakisikia adhana wanaweka silaha zao chini na kwenda kuabudu humohumo Hekaluni. 
Wakishamaliza ibada wanarudia silaha na kuanza kutwangana tena. Watanzania hawajazoea vita. Kwa mila na tamaduni zetu, huwezi kumdhuru mtu asiyekuhusu. Mkitwangana wenyewe kwa wenyewe mtajikuta mnazikana wenyewe kwa wenyewe; wajomba, wakwe, mashemeji na kadhalika.

Tuna tofauti kubwa na wenzetu waliojitenga kwenye jamii kwa vigezo vya udugu. Kuna sehemu ambazo huwezi kuoa mtu asiye nasaba yako, kama kule wanakooana wapwa na mabinamu.

Kwa kutokuzoea vita, tunajikuta tukikimbilia kwenye matukio ya hatari. Hapo Kongo DRC tairi ya gari ikipasuka, watu wanazama mafichoni. Tofauti na sisi ambao mabomu yalipolipuka Mbagala na Gongo la Mboto, askari walilazimika kutumia nguvu za ziada kuwatimua wananchi waliokuwa wakikimbilia kushuhudia. Bado hatujajua kuwa yapo mabomu yanayolipuka mfululizo: baba, mtoto, mjukuu, kitukuu, kilembwe hadi kining’ina.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *