Rais wa Marekani Donald Trump amependekezasiku ya Ijumaa, Oktoba 17, kwamba itakuwa mapema kuipatia Ukraine makombora ya Tomahawk wakati wa ziara ya Rais Volodymyr Zelensky katika Ikulu ya White House. Rais wa Ukraine amesema Rais wa Urusi Vladimir Putin “hayuko tayari” kwa amani, huku Donald Trump akitaja kinyume chake.

Imechapishwa:

Dakika 2 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Rais wa Ukraine aliwasili mwendo wa saa 11:30 Ijumaa jioni kwa ziara yake ya tatu katika Ikulu ya White House tangu Rais Trump arejee mamlakani. Wakati huu, wawili hao waliketi pamoja na wasaidizi wao.

Alilakiwa na Donald Trump, ambaye alipiga naye picha kwa muda mfupi kabla ya kuingia ndani ya jengo hilo. Wakati wa mkutano huo, Volodymyr Zelensky alisema Rais wa Urusi Vladimir Putin “hayuko tayari” kwa amani, huku Donald Trump akiamini kinyume chake. “Nadhani Rais Putin anataka kumaliza vita,” Donald Trump alitangaza wakati akimkaribisha mwenzake wa Ukraine katika Ikulu ya White House.

“Tunahitaji Tomahawks,” Volodymyr Zelensky alimwambia Donald Trump, kuhusu makombora haya yenye masafa ya kilomita 1,600 ambayo yangeiruhusu Ukraine kushambulia Urusi kwa kina, akipendekeza mabadilishano na “maelfu” ya ndege zisizo na rubani za Ukraine.

Rais wa Marekai alibainisha itakuwa mapema kuipatia Ukraine makombora ya Tomahawk, linaripoti shirika la habari la AFP. “Natumai hawazihitaji. Natumai tunaweza kumaliza vita bila kufikiria kuhusu Tomahawk,” Donald Trump aliwaambia waandishi wa habari.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky alimpa mwenzake wa Marekani Donald Trump “ramani” wakati wa mkutano wao mjini Washington unaoonyesha maeneo yanayoweza kulengwa nchini Urusi, chanzo kimoja ndani ya ujumbe wa Ukraine kilisema.

Viongozi wa Urusi na Marekani walikubaliana kukutana hivi karibuni mjini Budapest, Hungary. Donald Trump alikiri kwamba mwenzake wa Urusi anataka kukimbizana na wakati katika mzozo wa Ukraine, huku akibainisha kwamba Vladimir Putin anataka makubaliano. Alipoulizwa iwapo ana wasiwasi kwamba rais wa Urusi anajaribu kupoteza wakati, Donald Trump alijibu: “Ndiyo, nina wasiwasi,” alisema na kuongeza: “Lakini nadhani mimi ni vizuri sana katika jambo la aina hii. Nadhani anataka kufanya makubaliano.”

Wakati majira ya baridi yanapokaribia, Urusi inazidisha mashambulizi yake kwenye miundombinu ya nishati ya adui. Siku ya Ijumaa, pia ilidai kutekwa kwa vijiji vitatu vya Ukraine katika majimbo ya Kharkiv na Dnipropetrovsk.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *