Karibuni wasikilizaji wapendwa wa Idhaa ya Kiswahili Redio Tehran katika makala yetu ya wiki hii ambayo tumewaandalia kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Vipofu na Fimbo Nyeupe Duniani; siku ya kusherehekea irada, uhuru na utu wa watu wasioona au vipofu na kuanzishwa jitihada za kisayansi, kiteknolojia na kijamii nchini Iran na ulimwenguni kwa ujumla ili kuwaandalia jamii ya watu hao maisha rahisi na bora zaidi.

Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe (White Cane Safety Day) ni siku maalumu ambayo huadhimishwa kwa ajili ya watu wenye ulemavu wa macho (hasa vipofu). 
Fimbo nyeupe hutumiwa na watu wasiokuwa na uwezo wa kuona kuwaelekeza na kuwatambulisha kwa watumiaji wengine wa barabara, wakati wowote na hasa wanapokuwa wakitembea njiani. 

Wasikilizaji wapendwa tumewaandalia makala hii kwa mnasaba wa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe Duniani, siku ambayo inatukumbusha kuwa kuona si kwa macho tu; bali kuona kunamaanisha kutambua, kugusa na kuelewa ulimwengu unaotuzunguka. Ulimwengu ambao wakati mwingi hutumbukia gizani lakini unaendelea kung’aa kwa nuru ya mioyo.  

Katika kalenda ya kimataifa, tarehe 15 mwezi Oktoba kila mwaka inajulikana kama Siku ya Kimataifa ya Fimbo Nyeupe (White Cane Safety Day). Siku ambayo uhuru, uwezo na ujasiri wa vipofu na wale wenye matatizo ya kuona  huadhimishwa.  

James Biggs mpiga picha katika mji wa  Bristol, Uingereza kwa mara ya kwanza  mwaka 1921 alitumia fimbo nyeupe. Alipoteza uwezo wake wa kuona katika ajali na akatumia fimbo nyeupe kujiongoza wakati akitembea barabarani. Miaka kumi baadaye, mnamo mwaka 1931, huko Ufaransa, Guilly d’Herbemont aliwasilisha kwa vipofu fimbo mbili nyeupe kama nembo mbele ya mawaziri kadhaa wa nchi hiyo. Baada ya hapo karibu fimbo nyeupe elfu tano zilitumwa kwa walemavu na kwa watu waliopofuka wakati wa Vita vya Kwanza vya Dunia. Sambamba na nchini Marekani pia George A. Bonham mwanachama wa kundi la Lions Club aliiarifisha rasmi fimbo hiyo nyeupe. Kundi hilo lilivumbua fimbo nyeupe baada ya kipofu mmoja kujaribu usiku mmoja kuvuka barabara kwa kutumia fimbo nyepesi iliyokuwa na rangi nyeusi. Baada ya kushuhudia tukio hilo, wanachama wa Lions Club walimpatia fimbo nyeupe mtu huyo ili magari yaweze kumuona vizuri.

Mwaka 1931 Lions Club International ikawa programu ya kukuza usalama na matumizi ya fimbo nyeupe miongoni mwa vipofu. Utamaduni wa kutumia fimbo nyeupe kwa vipofu ulianza huko Illinois mwezi Desemba 1930, na madereva wakaitambua fimbo hiyo kama nembo ya kuwatambua wenye ulemavu wa macho (Wasioona).

Fimbo nyeupe ilitengenezwa na Dakta Richard E. Hoover katika Hospitali ya Jeshi ya Valley Forg wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ili kuwasaidia watu walioathiriwa na vita; fimbo hizo awali zilikuwa za kawaida tu na zilizotengenezwa kwa kutumia miti na kupakwa rangi nyeupe. Lakini ilipofika mwaka 1944 Dakta Hoover aliziarifisha fimbo  hizo kwa kundi la Lions Club na kuzifanyia kazi kwa takriban wiki moja na kisha kuzibadilisha na kuwa hizi zinazotambulika sasa kama Fimbo Nyeupe. Hoover alitengeneza fimbo ndefu za plastiki ambazo ndio msingi wa muundo wa sasa wa fimbo zinazotumiwa na vipofu kuwaongoza wakati wa kutembea. Baada ya uvumbuzi huu tajwa, DaktaHoover alijulikana kama baba wa ubunifu wa fimbo nyeupe. 

Karibu miongo miwili baadae mnamo Oktoba 15 1964 Kongresi ya Marekani ilisaini mswada na kuwa sheria ambapo bunge hilo liliarifisha tarehe 15 mwezi Oktoba kuwa Siku ya Fimbo Nyeupe. Tangu wakati huo, tarehe 15 Oktoba imearifishwa kuwa Siku ya Vipofu Duniani, ambapo fimbo nyeupe imechaguliwa kuwa alama ya kundi hili la watu. 

Fimbo nyeupe si wenzo tu bali ni nembo ya kuwa huru, ni nembo ya irada inayonena kuwa “Naweza kutembea, naweza kuishi, naweza kuchagua…”

Kila tunaposikia sauti ya fimbo nyeupe ikipiga chini, lazima tukumbuke kuwa sauti hii ni wimbo wa uhuru na utu wa mwanadamu.

Kwa mujibu wa ripoti za Shirika la Afya Duniani (WHO); zaidi ya watu milioni 285 duniani wanaishi na kiwango fulani cha upofu au uoni hafifu. 

Kati ya hao, karibu milioni 40 wamepoteza uwezo wa kuona kikamilifu. Hata hivyo kilicho na umuhimu si takwimu bali ni mtazamo wetu kuhusu suala hili.  Aghalabu ya watu wana mtazamo mzuri kuhusu maisha licha ya changamoto yao ya kuona. Ni watu mahiri na wenye kutia moyo katika nyanja kama vile muziki, elimu, teknolojia, michezo, saikolojia na hata usimamizi.

Huenda ukatamani kujua kwamba Louis Braille mvumbuzi Mfaransa aliyevumbua kile kinachochujulikana kama maandishi ya Braille  yaani (Nukta nundu) yeye pia alikuwa kipofu. 

Maandishi haya hutumiwa na watu wenye uoni hafifu au wasioona kabisa ili hatimaye waweze kusoma vitabu na majarida kama yale yaliyochapishwa kwa ajili ya watu wenye uwezo wa kuona. 

Watumiaji wa maandishi haya husoma kwa kupapasa nukta nundu hizo na hivyo kuweza kusoma kama watu wengine. 

Sawa na James Biggs, Louis Braille alipoteza uwezo wa kuona akiwa  mdogo sana, akiwa na umri wa miaka mitatu kutokana na ajali, lakini baadaye akavumbua njia iliyounganisha mamilioni ya vipofu kwenye ulimwengu wa maneno, sayansi na fikra.

Maandishi ya Braille si tu ni lugha bali ni ufunguo wa kuingia katika ulimwengu wa maarifa. Upofu siku zote haumaanishi kutoona. Wakati mwingine, macho hufunguka lakini miyo huwa imefungwa na wakati mwingine macho hujawa mwanga lakini akili hujawa na giza. Na wakati mwingine, wale ambao hawaoni wana macho zaidi kuliko aghalabu yetu.

Nchini Iran vipof ni sehemu ya jamii hodari na wachapakazi. Kwa miaka mingi, mashirika, taasisi, na mashirika mengi yamekuwa yakijishugulisha katika nyanja za elimu, ajira, michezo kwa kutoa msaada wa kijamii kwa wapendwa hawa tajwa. Wanafunzi wasioona wanasoma katika Vyuo Vikuu kote nchini, hufaulu katika nyanja za kitamaduni na kisanii, na wakati mwingine ni miongoni mwa wanaofanya vizuri katika nyanja kama muziki, isimu na sheria. Katika miaka ya hivi karibuni, teknolojia za kidijitali na vifaa mahiri vimewaandalia fursa mpya kwa ajili ya uhuru na uwepo wao katika jamii.

Iwapo utamuona mwanaume au mwanamke akitembea mtaani kwa kuongozwa na  fimbo nyeupe, ujue kwamba fimbo hiyo ni ishara ya jitihada zao za kuishi maisha ya kujitegemea na ya heshima. Mtu huyu hahitaji huruma bali heshima. Msaada wetu mkubwa kwa vipofu si kuwashika mkono, bali kuwaandalia njia ya maisha  na kuheshimu uwezo wao.

Fimbo nyeupe inapoonekana mkononi mwa kipofu, inamkumbusha kila mmoja wetu  kwamba “Mimi Sioni, lakini nipo; Sina kizuizi, na mimi ni sehemu ya jamii.” Fimbo hiyo nyeupe aidha inaweza kutajwa kama ishara ya tahadhari kwa madereva na watembea kwa miguu; kumfungulia njia mtu anayekanyaga njia yake gizani (kipofu) kwa hekima na ujasiri.

Kila tunapomwona kipofu akitembea kwenye njia yake uzima na fimbo yake nyeupe, tukumbuke kuwa yeye ni ishara ya utashi wa mwanadamu. Fimbo yake nyeupe si ishara ya kizuizi; bali ni ishara ya matumaini, uhuru, na imani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *