Dar es Salaam. Wimbi la mikopo ya simu limebadilisha maisha ya Watanzania wengi, hasa wale wanaoishi mijini, ambao kwa sasa kumiliki simu janja si jambo la anasa tena bali ni sehemu ya maisha ya kila siku.

Huduma hizi zimewapa wananchi fursa ya kununua simu bora kwa malipo ya awamu, hatua iliyoongeza kasi ya upatikanaji wa vifaa vya mawasiliano nchini na kuongeza ushiriki wao katika uchumi wa kidijitali.

Kigezo kikubwa cha kupata simu hizo ni uwe na kianzio, pamoja na kitambulisho cha Taifa (Nida).

Ripoti ya Takwimu ya Sekta ya Mawasiliano inayoishia Juni 2025 inaonyesha Tanzania kuna simu janja 25,048,038. Hatua hii muhimu katika mchakato wa mageuzi ya utoaji wa huduma za mawasiliano na huduma za kifedha kupitia simu.

Asha Mussa (29), mamalishe eneo la Kisemvule, mkoani Pwani ni miongoni mwa wanufaika wa mikopo ya simu janja.

Awali alikuwa anatumia simu ya kawaida maarufu tochi aliyoutumia kwenye kupiga, kupokea simu na jumbe pekee lakini sasa dunia ipo kiganjani mwake baada ya kuichangamkia fursa ya kupata simu janja kwa mkopo.

Asha alichagua simu janja yenye thamani ya Sh450,000. Akalipa Sh50,000 kama amana, kisha akaanza kulipa Sh10,000 kila wiki.

“Nilihofia nisingeweza kumaliza kulipa, hata hivyo nilimaliza mkopo kwa miezi minane tu. Ninachokipata sasa ni kikubwa zaidi ya zamani. Simu imenifanya nifanye biashara ya kisasa,” anasema.

Joseph Lema (33), dereva wa bodaboda ni mfano mwingine wa namna simu zitolewazo kwa mkopo imebadilisha maisha yake, akieleza awali alikuwa nayo ya kawaida ambayo haikumuwezesha kufanya usafirishaji kwa njia ya mtandao.

“Niliposikia inawezekana kukopa simu nikaona na mimi nitumie fursa hiyo, sasa napata wateja wengi. Simu imenifungulia dunia mpya. Naweza kuona ramani, kupata wateja haraka na hata kufanya malipo kwa simu. Sijawahi kuchelewa kulipa mkopo wangu kwa sababu simu hii inanilipa kila siku,” anasema.

Neema Marwa, mwanafunzi wa chuo anasema alikopa simu kupitia kampuni ya mikopo mtandaoni ili kufanikisha masomo yake.

“Nilihitaji simu fulani iliyokuwa inauzwa Sh900,000 sikuwa na uwezo wa kupata fedha hiyo kwa wakati mmoja ikabidi nikope. Nilipata simu kwa mkopo wa miezi sita. Ingawa marejesho ni changamoto, lakini nilifanikiwa na inanisaidia katika mambo yangu mbalimbali ikiwemo kwenye elimu,” anasema.

Changamoto zilizopo

Wafanyabiashara wa vifaa vya simu wanakiri mfumo wa mikopo umeongeza mauzo yao maradufu.

Fatuma Ally, muuzaji wa simu Vikindu, anasema awali kabla ya kuanza mpango wa mikopo, alikuwa anauza simu zisizozidi 10 kwa wiki, lakini sasa anauza zaidi ya 30.

“Watu wengi wanakuja kwa sababu wanaona hata kama hawana pesa zote, wanaweza kupata simu na kulipa taratibu. Hii imetusaidia sisi wafanyabiashara kuongeza mauzo na faida,” anasema.

Kampuni zinazotoa huduma za mikopo zimeajiri vijana wengi kama mawakala wa mauzo, jambo lililoongeza ajira.

Pamoja na mafanikio haya, wakopeshaji wanakiri changamoto zipo.

Benson Malema, mfanyabiashara wa simu Kisemvule, anasema zaidi ya asilimia 20 ya wateja huchelewa kulipa mikopo.

“Wengine wanauza simu walizokopeshwa kabla ya kumaliza malipo. Kuna wanaozima laini kabisa na kupotea. Hii inatufanya tuweke mifumo ya kudhibiti, ikiwemo kufunga simu endapo deni halijalipwa,” anasema.

Changamoto nyingine ni uelewa mdogo wa mikataba kwa kile anachoeleza baadhi wa wateja hukiuka masharti.

“Unapokopa kuna masharti unapewa lakini unakuta mtu anakiuka, ukweli ni kwamba wengi ni waaminifu ila hawakosekani wachache na inapotokea unakuwa huna budi zaidi ya kuifanya simu hiyo isiweze kutumika,” anasema pasipo kutaka kuingia kwa undani kuhusu hilo.

Kwa upande wa wakopaji, wapo wanaolalamika kuhusu riba kubwa na adhabu endapo wanachelewa kulipa kama anavyoeleza Asha, kwamba ilibidi ajitume sana ili apate fedha za kumaliza mkopo kwa wakati.

“Nafahamu watu ambao wameshakutana na rungu la kufingiwa simu kwa sababu ya kuchelewesha marejesho, ilibidi mimi nipambane ili yasinikute hayo. Biashara ingesuasua, ningeshindwa kulipa. Lakini nilijua simu ni muhimu, nikajitahidi. Wengine hawana bahati hiyo,” anasema.

Faida za kiuchumi

Mchambuzi wa uchumi Regina Msuya, amesema mikopo ya simu janja imerahisisha ujumuishaji wa kifedha na kuongeza mchango wa sekta ya mawasiliano katika Pato la Taifa na kupunguza pengo la upatikanaji wa teknolojia kati ya wenye kipato cha chini na cha juu.

“Simu janja si kifaa cha mawasiliano tu bali ni nyenzo ya uzalishaji na lango la uchumi wa kisasa. Watu wengi sasa wanatumia simu kufikia masoko, kupata taarifa za bei, kufanya biashara na hata kuomba mikopo.

“Mamalishe sasa anaweza kupokea pesa kwa njia ya simu, kijana wa bodaboda anapata wateja kupitia mtandao na mfanyabiashara mdogo anauza bidhaa kupitia mitandao ya kijamii. Hii imeongeza uzalishaji na mapato,” anasema.

Kwa mujibu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), sekta ya mawasiliano ilikua kwa asilimia 9.2 mwaka 2024, ikichangia zaidi ya Sh3.5 trilioni kwenye uchumi wa Taifa.

Kupitia umiliki wa simu janja, idadi ya watu wanaotumia huduma za kifedha imeongezeka maradufu ambapo Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaeleza kuwa zaidi ya asilimia 76 ya Watanzania sasa wanatumia huduma za kifedha kupitia simu, ikilinganishwa na asilimia 65 mwaka 2022.

Hali hii imerahisisha upatikanaji wa mikopo midogo, uwekezaji wa hisa, bima na huduma za malipo ya kodi kwa njia ya mtandao.

Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi wa Mawasiliano Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mulembwa Munaku, amekiri kuwa bila ya kuongeza njia mbalimbali za upatikanaji wa simu janja, ikiwemo mikopo, idadi ya ongezeko la simu hizo lisingefikiwa kwa haraka.

“Japo idadi ya wanaomiliki simu janja bado ni ndogo lakini tunatambua zipo njia mbalimbali zinazochangia simu hizi kuendelea kuongezeka ikiwemo hii ya mikopo na inafanyika si tu Tanzania bali mataifa mengi, lengo likiwa kuwawezesha wananchi wale wa kipato cha chini wasiachwe nyuma,” amesema.

Amesema hivi sasa simu janja ni kila kitu, huduma mbalimbali zinapatikana. Kwa kifupi, mambo mbalimbali yamerahisishwa na simu janja na ndiko uliko uchumi wa kidijitali.

“Hivyo tunaunga mkono jitihada zote zinazoendelea kufanyika kuhakikisha Watanzania wengi wanaweza kumiliki simu hizi,” amesema.

Kuhusu malalamiko ya riba na utaratibu wa mikopo hiyo Munaku amesema: “Sisi tunasimamia sekta ya mawasiliano masuala ya mikopo yanaratibiwa na BoT na uzuri wamekuwa wakitoa miongozo kuhakikisha riba haziwaumizi wakopaji.”

“Tukiwa wadau wakubwa tutaendelea kushirikiana na BoT kuona kama kuna maeneo yanahitaji kuboreshwa au kuwekewa miongozo zaidi,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *