Dar es Salaam. Yanga imejipanga kuhakikisha inapata ushindi katika mchezo wa ugenini dhidi ya Silver Stikers ya Malawi leo kwenye Uwanja wa Bingu ili isiwe na kibarua kigumu katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika utakaochezwa Dar es Salaam, Tanzania mwishoni mwa wiki ijayo.

Kocha Mkuu wa Yanga, Romain Folz amesema licha ya upinzani ambao wanategemea kuupata kutoka kwa Silver Strikers, wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na ushindi katika mechi hiyo iliyopangwa kuanza saa 10:00 jioni kwa muda wa Tanzania.

“Tumejiandaa vizuri kuelekea mchezo wetu wa kesho na leo jioni tutapata nafasi nyingine ya mwisho ya maandalizi.  Tumeangalia historia ya wapinzani wetu na kufanya utafiti wa kiufundi kama tunavyofanya tukikutana na wapinzani wengine.

“Hakuna mchezo mrahisi au mpinzani mwepesi kwenye mashindano makubwa na tumejiandaa vizuri kwa hilo kwasababu kila mchezo ni muhimu na ndiyo namna tutauendea mchezo kuhakikisha tunaondoka hapa na matokeo mazuri,” amesema Folz.

Hii ni mara ya kwanza kwa Yanga kukutana na timu ya Malawi katika mashindano ya Klabu Afrika katika ushiriki wake wa kipindi cha miaka 56.

Hata hivyo, Julai, 2023, Yanga ilicheza mechi ya kirafiki na Nyasa Big Bullets kwenye Uwanja huohuo wa Bingu utakaochezewa mechi ya leo na timu hizo zilitoka sare ya bila kufungana.

Mchezo huo wa kirafiki ulikuwa ni wa kusherehekea Kumbukumbu ya Uhuru wa Malawi ambapo Yanga ilipata mualiko rasmi kutoka kwa serikali ya nchi hiyo.

Timu hizo zinakutana huku zikiwa na mwenendo tofauti katika siku za hivi karibuni huku Yanga ikionekana kufanya vyema kuliko Silver Strikers katika mechi za hivi karibuni.

Kumbukumbu ya mechi tano zilizopita za mashindano tofauti, inaonyesha Yanga imepata ushindi mara nne na kutoka sare moja huku Silver Strikers ikipata ushindi mara mbili, droo mbili na imepoteza moja.

Katika hatua nyingine, Yanga jana usiku ilifanya tukio maalum la kumkumbuka kocha wao wa zamani, Marehemu Jack Chamangwana kwa kutoa cheti cha shukrani pamoja na zawadi ya fedha kwa mjane wa kocha huyo.

Tukio hilo liliongozwa na Rais wa Yanga, Hersi Said aliyeambatana na uongozi na kikosi cha timu hiyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *