
Tom Fletcher, Mwakilishi wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Misaada ya Kibinadamu, amesema kuwa, kiwango cha uharibifu katika Ukanda wa Gaza haikitasawariki kiasi kwamba, ni vigumu kuamini hali hiyo kwani kila kitu kimeharibiwa kabisa.
Kwa mujibu wa Shirika la Habari la Iran Press, Fletcher ameongeza kuwa Umoja wa Mataifa umeandaa mpango wa kina wa siku 60 wa kutoa msaada kwa Gaza, ambao mwanzoni utajumuisha kuwasili kwa misaada ya kibinadamu. Mpango huo ni pamoja na kutoa mikate, kupeleka mahema, na kuboresha usafi wa mazingira na majitaka.
Mwakilishi huyo wa Umoja wa Mataifa amesisitiza kuwa ujenzi wa hospitali na skuli ni hitajio la dharura katika eneo hilo, na kwamba hatua za kina zinahitajika kwa ajili ya ujenzi kamili wa Gaza.
Vile vile ametoa wito wa kufunguliwa vivuko vyote vya mpaka wa Gaza na kusema kuwa, maelfu ya malori yanayobeba misaada ya kibinadamu yanapaswa kuingia katika eneo hilo; mchakato wa kuingia kwa malori haya umeanza na athari yake chanya inaonekana.
Tom Fletcher ameeleza kuwa, majukumu ya Umoja wa Mataifa katika hatua hii ni mazito sana, akisema hata kutoa miili kutoka kwenye vifusi kunahitajia vifaa vingi.
Mapema mwezi huu, utawala wa Israel na harakati ya Muqawama wa Kiislamu ya Palestina (Hamas) zilikubaliana kutekeleza awamu ya kwanza ya mpango ya kusitisha vita Gaza; mpango ambao unatarajiwa kuhitimisha vita vya mauaji ya kimbari vya zaidi ya miaka miwili yaliyoanzishwa na Israel dhidi ya wakazi wa Ukanda wa Gaza.