
Chanzo cha picha, Reuters
-
- Author, Roncliffe Odit
- Nafasi, BBC News Swahili
Maelfu ya waombolezaji leo Jumamosi walikusanyika katika jiji la Kisumu, Kenya, kutoa heshima zao za mwisho kwa Waziri Mkuu wa zamani, Raila Odinga.
Mwili wa mwanasiasa huyo aliyekuwa na umri wa miaka 80 sasa umewekwa katika uwanja uliopo kwenye jiji ambalo alikuwa na ushawishi mkubwa, baada ya mazishi ya kitaifa yaliyofanyika siku ya Ijumaa jijini Nairobi, siku mbili baada ya kufariki katika hospitali moja nchini India.
Watu kadhaa wamejeruhiwa wakati umati uliposogea mbele kuangalia jeneza, na sasa wanapatiwa matibabu na maafisa wa huduma ya kwanza mahali hapo.
“Nimekuja hapa kumuomboleza kiongozi nyota wa Afrika,” alisema mmoja wa waombolezaji, Dixon Ochieng, akizungumza na BBC, huku wengine wakisikika wakilia na kuimba, “sisi ni yatima” kutokana na huzuni yao.
Watu wa rika zote walianza kufika katika Uwanja wa Jomo Kenyatta jijini Kisumu kabla ya alfajiri siku ya Jumamosi kwaajili ya kutoa heshima zao za mwisho.
Wengi walivaa nguo zenye rangi ya chungwa, ambayo ni rangi ya chama chake cha Orange Democratic Movement (ODM), huku wakipunga matawi. Hii ni ishara ya jadi ya maombolezo na huzuni miongoni mwa jamii ya kabila la Waluo, ambayo Odinga alikuwa ndio asili yake.

Odinga alikuwa kiongozi mkuu wa upinzani nchini Kenya kwa miaka mingi, akiwa ameshindwa katika kampeni tano za kugombea kiti cha urais, ile ya hivi karibuni kabisa ilikuwa miaka mitatu iliyopita. Mara kwa mara alisema alidhulumiwa ushindi wake, akidai kuwepo kwa ulaghai katika kura za uchaguzi.
Baada ya uchaguzi wa 2007 uliogubikwa na pingamizi na damu kumwagika, aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu katika serikali ya umoja wa kitaifa.
Anachukuliwa kuwa mmoja ya watu muhimu walioanzisha mfumo wa demokrasia wa vyama vingi nchini Kenya na ana wafuasi wengi wa dhati katika sehemu za Magharibi mwa nchi hiyo.
“Ninamkumbuka kwa kutupa demokrasia, kwa kunipa uhuru wetu, na sasa tuna uwezo wa kuzungumza na kusema chochote tunachokiona kuwa ni kibaya kwetu,” Jacob Omondi aliiambia BBC kuhusu mchango wa Odinga katika nchi.
Mwombolezaji mwingine, David Ouma, alisema: “Nilijifunza kutoka kwa Raila kuwa na uvumilivu, kwasababu Raila alikuwa kiongozi mwenye uvumilivu mkubwa kwenye kila uchaguzi… bado aliweza kusimama na kujaribu tena na tena.”

Miongoni mwa viongozi waliotoa heshima kwa Odinga alikuwa Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ambaye familia yake ya Kenya pia inatokea katika eneo hilo.
“Raila Odinga alikuwa shujaa wa kweli wa demokrasia. Ishara ya uhuru, alivumilia miongo mingi ya mapambano na kujitolea kwasababu pana ya kuwa na uhuru na nchi kujiongoza na kusimamia masuala yao wenyewe bila kudhibitiwa na mamlaka za nje,” Bwana Obama aliandika kwenye mtandao wa kijamii wa X.
“Mara kwa mara, mimi binafsi nilimuona akiweka maslahi ya nchi yake mbele ya maslahi yake binafsi. Kama viongozi wachache wa aina hii popote pale, alikuwa tayari kuchagua njia ya upatanisho wa amani bila kupunguza au kubadilisha maadili yake ya msingi,” alisema Bwana Obama.
Odinga anatarajiwa kuzikwa siku ya Jumapili baada ya mazishi yatakayo hudhuriwa na watu wachache katika shamba lake huko Bondo, umbali wa takriban kilomita 60 (maili 40) Magharibi mwa Kisumu.
Kulingana na familia, aliomba kuzikwa haraka iwezekanavyo, ikiwezekana ndani ya saa 72.
Imetafsiriwa na Elizabeth Kazibure na kuhaririwa na Ambia Hirsi