Katavi. Samia Suluhu Hassan, mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ameahidi kuufanya Mkoa wa Katavi kuwa njia kuu ya biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa kuimarisha miundombunu ili mizigo kati ya mataifa hayo ipitie Ziwa Tanganyika.
Amesema wameshafanya usanifu ili kuboresha reli ya Kaliua -Mpanda yenye urefu wa kilomita 210, ili kupunguza muda wa usafiri kutoka saa saba hadi nane na kuwa saa mbili hadi tatu.
Hatua hiyo amesema itachochea maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Katavi kupitia uboreshaji wa miundombinu, ikiwemo barabara na madaraja.
Samia, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anayemaliza muda wake ameahidi hayo leo Jumamosi Oktoba 18, 2025 katika mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Azimio, uliopo Mpanda mjini.
Amesema mikoa ya Katavi na Rukwa imefunguliwa kwa njia za barabara, anga, reli na usafiri wa kwenye maji. Pia wameimarisha huduma za jamii na kuwawezesha wananchi kiuchumi.
Amesema katika kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji wamekamilisha ujenzi wa Bandari ya Karema katika mwambao wa Ziwa Tanganyika uliogharimu Sh47.9 bilioni.
Amesema ujenzi huo wa bandari utarahisisha usafirshaji wa abiria na mizigo kati ya Tanzania na nchi jirani ikiwamo DRC, Burundi na Zambia.
“Ujenzi wa bandari unaenda sambamba na meli mpya za mizigo katika Ziwa Tanganyika na kazi hii inandelea vizuri pia. Kuelekea mwaka 2025/30 tunataka kuona biashara kubwa kati ya Tanzania na DRC inapita katika Bandari hii ya Karema,” amesema.
Mgombea huyo amesema kwa kuwa usafiri wa kwenye maji na reli unaambatana wameshafanya usanifu kwa ajili ya maboresho ya reli ya Kaliua- Mpanda ili kupunguza muda wa kusafiri.

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda.
Kuhusu barabara, Samia amesema zipo ikiwamo muhimu inayounganisha Wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi na ya Uvinza mkoani Kigoma, inayojengwa kwa kiwango cha lami kutoka Mpanda -Uvinza hadi Kanyani yenye urefu wa kilomita 250.4, ujenzi uliofikia asilimia 13.7 ikiwa inajengwa kwa vipande vinne na kuahidi atahakikisha inajengwa kwa kasi na kukamilika.
Mbali ya hayo, ameahidi Serikali itajenga barabara nyingine zilizoainishwa kwenye ilani ambazo ni muhimu kwa uchumi wa mkoa huo.
“Nafahamu kuna uhitaji wa madaraja katika maeneo muhimu na yanaendana na ujenzi wa barabara, katika miaka mitano ijayo pia tunaenda kujenga daraja la Kakese, Ugala na madaraja madogo na kubwa kuunganisha Manispaa ya Mpanda na Halmashauri ya Wilaya Nsimbo katika mto Mpanda eneo la Kakese katika Manispaa ya Mpanda,” amesema.
Kuhusu madai ya fidia, amesema ana taarifa ya uwepo wa madai hayo kwa wananchi waliopisha miradi ya maendeleo, wakiwamo 243 waliopisha ujenzi wa barabara ya Mpanda – Vikonge iliyokamilika 2021.
Amesema wananchi wengine 830 wanadai fidia kwa kupisha ujenzi wa barabara ya Mpanda hadi Sitalike.
Ameahidi kuelekeza Wizara ya Ujenzi kufanya upembuzi wa madai yatakayothibitika kuwa halali yatalipwa.
Amesema kufungua mkoa huo ni pamoja na kuimarisha huduma za mawasiliano, akisema mkoa wa Katavi una minara 64 na 63 imekamilika na inatoa huduma. Hivyo, wataendelea kuboresha huduma hasa kwa baadhi ya vijiji vya Wilaya ya Tanganyika.
Kuhusu sekta ya kilimo, amesema Serikali ilifanya uwekezaji mkubwa ili kuongeza uzalishaji, hivyo wataendelea kutoa ruzuku, ujenzi wa skimu za umwagiliaji na masula mengine ili kuongeza uzalishaji.
“Ninalotaka kulisema kwa mahususi ni kuwa tulijenga vituo vinne vya kukusanya na kuchakata mazao ya nyuki ili kuimarisha ufugaji wa nyuki zaidi, kwenye hili nimpongeze kaka yangu Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda kwa uhamasishaji na kuwa kinara wa uzalishaji asali,” amesema.
Akizungumzia sekta ya uvuvi ameahidi kujenga mabwawa, vizimba na vituo vipya na ukuzaji wa viumbe maji katika Ziwa Tanganyika ili kutoa fursa ya ajira kwa vijana.
Kuhusu viwanda amesema ilani ya chama hicho inaelekeza ujenzi wa kongani za viwanda kila wilaya na kila wilaya ijiandae kwa ajili ya viwanda vidogo na vya kati ambavyo vitaongeza thamani ya mazao yanayopatikana eneo husika.
“Miaka mitano iliyopita tulianza na viwanda vitano vikubwa na viwanda vya kati 20 mkoani Katavi na jumla ya ajira ndani ya viwanda hivyo ni 5,828. Hivyo tutajipanga kuongeza ajira kwa vijana kupitia uwekezaji wa viwanda ndiyo maana tunajenga vyuo vya Veta,” amesema.
Alichosema Dk Mwigulu
Mgombea ubunge Iramba Magharibi na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba, amesema Samia ameimarisha uchumi tangu mwaka 2021 alipochukua madaraka, akieleza kwa sasa Tanzania ina akiba ya Dola za Marekani 6.7 bilioni ambazo ni sawa na Sh16 trilioni.

Mgombea ubunge Iramba Magharibi na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Amesema baadhi ya watu wanapotosha kuwa Serikali inachapisha fedha, hivyo amewataka Watanzania kuwapuuza kwani madai hayo siyo ya kweli.
“Nakasikia wengine wanaongelea kwamba Serikali inachapisha hela, tuna akiba ya zaidi ya Sh16 trilioni. Hakuna nchi hata moja ina mtambo wake wa kuchapisha fedha ili itumie yenyewe duniani kote kwani fedha utaratibu wake mpaka uchapishe inakuchukua miaka miwili, unawezaje kuchapisha fedha baada ya kuingia kwenye uchaguzi,” amehoji na kuongeza:
“Wanadhani fedha unatoa nakala? karatasi ya fedha siyo nakala ‘photocopy’ wala hamna nchi inayochapisha hela. Niwaombe Watanzania mkiona mtu anakuelekeza jambo baya dhidi ya nchi yako, wakati hatuna nchi mbadala wa hii tujumuike tulinde amani.”
Katika hatua nyingine ameiomba jamii hasa wafugaji kila mmoja kujitokeza kwenda kupiga kura Oktoba 29, 2025 badala ya kutuma mwakilishi.
“Wafugaji tuna kawaida ya kutuma uwakilishi kupiga kura, niwaombe jambo, kura hatutumi mwakilishi twendeni wote tukapige kura, akienda mkuu wa kaya haimaanishi amewakilisha familia nzima,” amesema.
Awali, Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda, amesema kutokana na Mkoa wa Katavi kuwa na ukubwa kijiografia, amepitia ilani ya CCM ya 2025/30 na kuona maono ikiwemo ukuzaji wa sekta ya kilimo kupitia skimu za umwagiliaji na kuwa itakuza sekta hiyo.
Ameomba Serikali kusaidia vijana kupitia mradi wa Jenga Kesho iliyo Bora (BBT).
“Nimeona maono ya ilani kuhusu wafugaji na sekta nyingine. Eneo la mkoa wetu kubwa ni Hifadhi ya Taifa Katavi, hifadhi za misitu na mapori ya akiba, tuwezeshwe namna ya kutumia maeneo haya kwa ajili ya uwekezaji wa viwanda vya kuchakata mazao, kilimo na shughuli zingine ili mkoa uzidi kung’aa,” amesema.