#HABARI: Wanaushirika nchini wametakiwa kuendelea kulinda na kudumisha tunu ya amani iliyopo kwani ndiyo msingi wa maendeleo na ustawi wa vyama vya ushirika pamoja na taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa na Mwenyekiti wa Chama Kikuu cha Ushirika wa Wilaya za Masasi, Mtwara na Nanyumbu (MAMCU LTD), Alhaj Azam Mfaume Julajula, ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Mradi wa Pamoja wa Vyama Vikuu vya Ushirika wa Korosho (KCJE LTD), wakati wa ziara ya viongozi wa KCJE katika Chama Kikuu cha Ushirika cha CHATO.

Alhaj Julajula amesema amani ni nguzo kuu ya mafanikio katika sekta ya ushirika na kwamba kila mwanaushirika ana wajibu wa kuhakikisha anailinda kwa vitendo.

Ameeleza kuwa ziara hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa kanuni ya sita ya ushirika, ambayo inahimiza wanaushirika kutembeleana na kubadilishana uzoefu katika kujenga uwezo wa taasisi zao.

Pamoja na hayo Julajula amewataka wakulima kuendelea kutumia mfumo wa stakabadhi za ghala (WRRB)na kufanya mauzo kwa njia ya kidijitali kupitia Soko la Bidhaa Tanzania (TMX), amesema mfumo huo umeongeza uwazi na ushindani wa bei katika soko la mazao.

Ziara hiyo ya KCJE LTD inalenga kuimarisha ushirikiano na kubadilishana uzoefu kati ya vyama vikuu vya ushirika nchini, sambamba na kujenga misingi imara ya uendelevu katika sekta ya ushirika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *