
“Katika dunia hii ambayo mambo yanazidi kuwa magumu, hiki ndicho kinachostahili: ni nguvu pekee inayohifadhi amani,” alisema Merz Alhamis wakati akitoa hotuba kuhusiana na sera ya kigeni katika bunge la Ujerumani, Bundestag.
“Na udhaifu unaifanya amani iyumbe,” aliongeza Merz.
Kansela huyo aliwafahamisha wabunge kuhusiana na kuhudhuria kwake hafla ya kutiwa saini kwa azimio la amani kati ya Israel na wanamgambo wa Kipalestina wa Hamas, huko Sharm el-Sheikh, ambako viongozi wa Misri, Qatar, Uturuki na Marekani walikuwa wanasimamia hatua hiyo ya upatanishi.
“Vitendo vya kisiasa vinaleta tofauti katika dunia hii, kwa uzuri au kwa mabaya,” alisema Merz. “Tangu Jumatatu ya wiki hii, kumekuwa na matumaini mapya ya amani ya kudumu katika eneo hilo.”
Merz amesema ili kuwa wapiganiaji amani duniani, Ulaya ni sharti iwe yenye nguvu.