Bariadi. Makamu Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema nchi ipo salama na amani imetawala, huku akiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki uchaguzi wa Oktoba 29, 2025 na kuwapigia kura wagombea wenye sifa, akisisitiza kuwa kwa nafasi ya urais, Samia Suluhu Hassan ndiye anayestahili kuendelea kuiongoza Tanzania.
Wasira amesema hayo jana Oktoba 17, 2025 alipokutana na viongozi wa CCM Wilaya ya Bariadi, mkoani Simiyu, ambapo alisisitiza kuwa upotoshaji unaoenezwa mitandaoni hauna ukweli, na kwamba baadhi ya watu wanashirikiana na nguvu za nje kuvuruga amani ya nchi.
“Wako watu wanaokerwa na amani ya nchi yetu na wanashirikiana na watu wa nje kutaka kuwavuruga. Siku hizi mitandao ya kijamii inasambaza habari za uongo, za kutisha, zinazowafanya watu waamini kuna shida. Mimi nimekuja kuwaambia nchi ipo salama kabisa, hakuna tatizo, zimebaki siku 10 tu twende tukapige kura,” amesema.
Amewataka viongozi wa CCM katika ngazi zote kuendelea kuhamasisha wananchi kujitokeza mapema asubuhi siku ya kupiga kura, ili watumie haki yao ya msingi kuchagua viongozi wanaowaamini.

“Nendeni muwaambie Watanzania wenzetu wajitokeze kwa wingi, wapige kura kwa amani. Mamlaka ya nchi yapo mikononi mwa wananchi, huu ndiyo wakati wao wa kukabidhi madaraka kwa watu wanaowaamini,” amesema Wasira.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuwachagua viongozi wenye uadilifu, uaminifu na rekodi nzuri ya utumishi kwa Watanzania.
“Hatuwezi kumpa madaraka mtu ambaye hatumjui, hana historia ya utumishi, chama chake kimeibuka tu leo. Ni hatari kukabidhi nchi kwa watu ambao hawana rekodi wala uelewa wa changamoto za Watanzania,” amesema.
Wasira amesema CCM imeendelea kuwa chama kinachotekeleza ahadi zake kwa vitendo, na kwamba chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, miradi mingi ya maendeleo imefanyika katika Wilaya ya Bariadi.
“Kwa mfano, kwa kipindi cha miaka minne na nusu ya Rais Samia, tumejenga shule za msingi 10 kutokana na ongezeko la watoto, madarasa 81 ya shule za msingi, sekondari nane mpya, na madarasa mapya 143 ya sekondari kwa fedha za Serikali bila kuchangisha wananchi. Hiyo ndiyo tofauti ya CCM, tunaahidi na tunatekeleza,” amesisitiza.
Mitano ijayo
Akizungumzia Ilani ya Uchaguzi ya CCM 2025–2030, Wasira amesema chama hicho kimejipanga kutatua changamoto za wananchi wa Bariadi katika sekta za maji, umeme na elimu.
“Tumeanza utekelezaji wa mradi wa maji kutoka Ziwa Victoria hadi Bariadi, Meatu, Kisesa na Maswa. Huu siyo mradi wa maneno, matenki yamejengwa na kazi inaendelea,” amesema.
Ameongeza kuwa Serikali pia imepanga kujenga kituo cha kupoza na kusambaza umeme katika mkoa huo ili kuondoa changamoto ya kukatika kwa nishati mara kwa mara.
Wasira amehitimisha kwa kuwataka wananchi wa Bariadi na Watanzania kwa ujumla kudumisha amani, kuamini katika chama chenye historia ya utekelezaji, na kutumia kura zao kuendeleza maendeleo yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais Samia.