
Rais wa zamani wa Marekani, Barack Obama, ameonyesha heshima zake kwa kiongozi wa upinzani wa Kenya, Raila Odinga, aliyefariki nchini India mapema wiki hii na anatarajiwa kuzikwa Jumapili.
Obama alimuelezea Odinga kama kiongozi ambaye “aliweka maslahi ya nchi yake mbele ya matamanio yake binafsi.”
Rais huyo wa zamani wa Marekani, ambaye baba yake alitoka Kaunti ya Siaya kando ya Ziwa Victoria – eneo lile lile ambako Odinga alizaliwa na atapumzishwa, alikumbuka kujitolea kwa Odinga kwa maisha yake yote katika kupigania uhuru na demokrasia.
“Raila Odinga alikuwa bingwa wa kweli wa demokrasia. Mtoto wa enzi ya uhuru, alivumilia miongo ya mapambano na kujitolea kwa ajili ya lengo kubwa la uhuru na kujitawala kwa Kenya,” alisema Obama katika taarifa yake.
“Mara kwa mara, nilimwona binafsi akiweka maslahi ya nchi yake mbele ya matamanio yake binafsi,” aliongeza.