
Israel ilikuwa imetishia kutoufungua mpaka wa Rafah na kupunguza misaada na vifaa vingine kwa sababu Hamas ilikuwa inarudisha miili polepole sana, na pia kitendo cha kuurudisha mwil mmoja kati ya minne ambao haukuwa wa mateka waliokuwa wakizuiliwa Gaza.
Wakati huo huo wapalestina wawili wameuawa katika Ukanda wa Gaza licha ya makubaliano ya kusitisha mapigano yakiwa yanaendelea. Wahudumu wa afya katika Ukanda wa Gaza wamesema watu hao wameuawa kwenye mashambulizi ya Israel katika eneo la mashariki mwa Gaza.
Jeshi la Israel limesema watu kadhaa walioshukiwa kuvuka mstari uliowekwa na kuwakaribia wanajeshi wa Israel walikiuka makubaliano ya kusitisha mapigano na hivyo Wanajeshi walifyatua risasi ili kukabiliana na kitisho hicho.
Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, amesisitiza kuwa Hamas lazima itimize masharti ya makubaliano ya kusitisha vita yaliyopendekezwa na Rais wa Marekani Donald Trump, ikiwemo kurejesha miili ya mateka waliokufa.
“Sawa, tulikubaliana kuipa amani nafasi. Tulikubaliana kuwa masharti ya mpango wake wa vipengele 20 ni wazi kabisa. Sio tu kwamba tunawapata mateka bila kuondoa jeshi letu, bali pia kwamba baadaye kutakuwa na hatua mbili: ya kwanza ni kuondoa silaha, na ya pili ni kuzuia uundaji wa silaha“
Netanyahu arejea Mahakamani
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amerejea tena katika mahakama ya mjini Tel Aviv kwa ajili ya kusikiliza kesi yake ya muda mrefu ya tuhuma za ufisadi,. Kesi hiyo ilifunguliwa mwezi Mei mwaka 2020.
Netanyahu na msafara wake wa mawaziri kadhaa kutoka kwenye chama chake cha kihafidhina cha Likud walipokuwa wakielekea kwenye mahakama hiyo walizomewa na waandamanaji.
Rais wa Marekani Donald Trump alipendekeza siku ya Jumatatu alipokuwa nchini Israel kwamba Waziri Mkuu huyo asamehewe kesi tatu tofauti za ufisadi zinazomkabili.