Timu zilizojikatia tiketi ya mashindano hayo moja kwa moja kutoka Afrika ni Algeria, Cape Verde, Misri, Ghana, Ivory Coast, Morocco, Senegal, Afrika Kusini, Tunisia.

Hii ndiyo mara ya kwanza kwa Cape Verde kufuzu kwenye mashindano hayo katika historia ya kandanda ya nchi hiyo na kwa Afrika Kusini, hii ni mara ya kwanza kufuzu tangu walipokuwa waandalizi mwaka 2010.

Kupunguziwa pointi kwa kuchezesha mchezaji haramu

Bafana bfana wamefuzu licha ya kuwa waliianza mechi ya Jumanne dhidi ya Rwanda wakiwa katika nafasi ya tatu nyuma ya Benin na Nigeria.

Afrika Kusini walikuwa wamepunguziwa pointi tatu kwa kumchezesha mchezaji asiye halali ila hilo halikuwazuia kujikatia tiketi ya moja kwa moja.

Mashabiki wa Afrika Kusini wakati wa mechi dhidi ya Namibia
Mashabiki wa Afrika Kusini wakati wa mechi dhidi ya NamibiaPicha: AP

Ushindi wao wa 3-0 dhidi ya Rwanda uliwapelekea kuchupa hadi katika nafasi ya kwanza na hatua ya Nigeria kupata ushindi mkubwa wa 4-0 dhidi ya Benin imewapelekea kumaliza wapili katika kundi C. Nigeria sasa wamejikatia nafasi ya kushiriki mechi za mchujo.

Iwapo Rwanda wangeifunga Afrika Kusini basi Nigeria wangemaliza wa kwanza na kufuzu moja kwa moja.

Nigeria, Cameroon, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo na Gabon sasa watacheza mechi za mchujo ambazo zitakuwa za mkondo mmoja tu kuamua atakayeshiriki mashindano mashindano ya mchujo wa kikanda yatakayofanyika huko Mexico mnamo mwezi machi 2026.

Sasa mpinzani katika mechi hizi za mchujo anajulikana kutokana na nafasi inayoshikilia timu katika orodha ya timu bora ya FIFA ambayo hutolewa kila mwezi na mwezi huu inatarajiwa kutolewa tarehe 23. Lakini orodha ya Septemba haitarajiwi kubadilika.

Timu inayoorodheshwa juu zaidi katika timu hizo nne zilizofuzu mchujo, itapambana na timu inayoorodheshwa chini zaidi halafu timu ya pili inayoorodheshwa juu icheze na timu ya pili inayoorodheshwa chini.

Nigeria yaorodheshwa juu katika FIFA

Kati ya timu nne zilizofuzu mchujo, Nigeria ndiyo inayoorodheshwa juu kabisa katika nafasi ya 45 duniani na timu inayoorodheshwa chini ni Gabon katika nafasi ya 79 kwa hiyo mpinzani wa Nigeria atakuwa Gabon, katika mechi itakayochezwa Novemba 13 nchini Morocco.

Mlinda lango wa Cameroon Andre Onana
Mlinda lango wa Cameroon Andre OnanaPicha: Heuler Andrey/IMAGO

Halafu Cameroon ni timu inayoorodheshwa ya pili kutoka juu katika nafasi ya 52 na itakabiliana na Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo iliyo katika nafasi ya 60 katika mechi ya mkumbo mmoja pia itakayogaragazwa huko huko Morocco.

Washindi wa mechi hizi mbili watacheza baina yao katika fainali huko huko Morocco mnamo Novemba 16 na mshindi atakuwa amepata nafasi ya kushiriki mechi nyengine za mchujo huko Mexico mnamo mwezi Machi.

Huo mchujo wa huko Mexico utakuwa ni mchujo wa mabara tofauti na timu mbili ndizo zitakazojikatia tiketi ya kushiriki Kombe la Dunia.

Mchujo huo utazileta pamoja jumla ya timu sita kutoka mashirikisho ya CAF, CONMEBOL, OCEANIA na ASIA ambapo timu mbili zitakazokuwa zinaorodheshwa juu kwenye orodha ya FIFA zitafuzu moja kwa moja kwenye fainali.

Hizo nne zilizosalia zitacheza nusu fainali baina yao na zitakazoshinda zitatinga fainali kisha washindi wa fainali hizo mbili watafuzu kwenye Kombe la Dunia.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *