
Kiongozi wa mapinduzi ya kijeshi nchini Madagascar, Kanali Michael Randrianirina, alisema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na Umoja wa Afrika, ambao siku moja kabla ulisimamisha uanachama wa nchi hiyo baada ya Rais Andry Rajoelina kuondolewa madarakani.
“Uamuzi huo ulitarajiwa. (Lakini) kuanzia sasa, kutakuwa na mazungumzo ya siri. Tutaona mambo yatakavyokwenda,” alisema katika mkutano na waandishi wa habari Alhamisi.
Randrianirina alisema atakula kiapo kama rais siku ya Ijumaa katika sherehe itakayofanyika na Mahakama Kuu ya Katiba katika mji mkuu, Antananarivo.
Hata hivyo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, siku hiyo hiyo alilaani kile alichokiita mabadiliko ya kikatiba yasiyo halali ya serikali katika nchi hiyo ya kisiwa, akitoa wito wa kurejeshwa kwa utawala wa kikatiba na sheria.