Maafisa usafirishaji (boda boda na bajaji) zaidi ya 1,000 wa jimbo la Mtumba mkoani Dodoma wamefanya maandamano ya kuweka wazi azma yao ya kushiriki katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29.
Bodaboda hao wameeleza dhamira yao mbele ya mgombea ubunge wa jimbo hilo Anthony Mavunde wakati wa shamrashamra za kampeni za mgombea ubunge huyo zilizofanyika kwenye mitaa mbalimbali ya jimbo hilo.
Mbali na kuweka wazi azma hiyo pia maafisa usafirishaji hao walitumia fursa hiyo kutoa shukran kwa Dkt. Samia kwa kuwajengea ofisi ya mkoa iliyopo kwenye eneo la Makole.
Naye mgombea ubunge wa jimbo hilo, Anthony Mavunde ameipongeza serikali kwa kuweka nguvu na mikakati ya kuiinua sekta hiyo ambayo imeendelea kuzalisha ajira nyingi kwa vijana hususani kwenye maeneo ya miji na majiji nchini na Afrika nzima.
Kando na shukrani hizo Mavunde amewaomba maafisa hao kumchagua katika Uchaguzi Mkuu na kuahidi kuchangia Shilingi Milioni 20 endapo atafanikiwa kushinda ubunge kwa ajili ya kutunisha mfuko wa SACCOS ya maafisa usafirishaji hao.
Mbali na ahadi hiyo Mavunde pia ameahidi kuwezesha upatikanaji wa mikopo ya tairi za pikipiki kwa uwezeshaji wa kutumia mfumo wa kulipa kidogo kidogo na ahadi nyingine za maendeleo.
Imeandaliwa na @moseskwindi