Wakati ripoti zikionyesha kuwa Pentagon inatayarisha machaguo ya kijeshi dhidi ya Venezuela, Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM), ambayo inaundwa na zaidi ya nchi 120, imeonya kwamba shambulio lolote dhidi ya nchi hiyo ya Amerika Kusini litakuwa ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa.
Mwishoni mwa kikao chao cha dharura mjini Kampala huko Uganda, mawaziri wa mambo ya nje wa Harakati ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote walitoa taarifa wakionya juu ya kushadidi hali ya wasiwasi katika Bahari ya Caribbean na uwezekano wa kutokea mashambulizi ya kijeshi ya Marekani dhidi ya Venezuela. Taarifa hiyo inaeleza kuwa, hatua yoyote ya kijeshi dhidi ya Venezuela ni ukiukaji wa wazi wa Mkataba wa Umoja wa Mataifa na kanuni za kutoingilia masuala ya ndani ya nchi nyingine, na inaweza kuhatarisha amani na utulivu wa eneo la Amerika ya Kusini.
Mawaziri wa mambo ya nje wa NAM wamesisitiza katika taarifa yao kwamba “mienendo ya uchochezi na vitisho vya kutumia mabavu dhidi ya mataifa huru ni kinyume na moyo wa ushirikiano wa kimataifa na itasababisha kuongezeka mivutano ya kijiografia na kuenea ukosefu wa usalama katika eneo la Caribbean.” Taarifa hiyo pia imelitaka Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukutana mara moja na kuamua juu ya matokeo ya uwezekano wa hatua za kijeshi za Marekani dhidi ya Venezuela.
Katika taarifa hiyo, Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote imeitaka serikali ya Marekani kuheshimu kanuni na sheria za kimataifa, ardhi za nchi mbalimbali, na haki ya watu kujitawala, na kujiepusha na uingiliaji wowote wa moja kwa moja au usio wa moja kwa moja katika masuala ya ndani ya Venezuela.

Mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa nchi wanachama wa NAM ulifanyika wakati ripoti zikisema kwamba, Pentagon inaandaa machaguo ya kijeshi dhidi ya Venezuela yatakayowasilishwa kwa Donald Trump. Vyanzo vilivyo karibu na Washington vinasema machaguo hayo yanajumuisha mashambulizi dhidi ya malengo ya kijeshi katika ardhi ya Venezuela na msaada kwa makundi yanayopinga serikali ya Caracas.
Rais wa Marekani, Donald Trump, pia hajakanusha uwezekano wa kufanyika mashambulizi ya kijeshi katika ardhi ya Venezuela, na huku akiashiria mashambulizi ya hivi karibuni ya Marekani dhidi ya boti karibu na pwani ya Venezuela, alisema: “Sasa tunachunguza ipasavyo chaguo la mashambulizi ya nchi kavu.”
Katika wiki za hivi karibuni, mashambulizi kadhaa ya kijeshi ya Marekani yamezamisha meli ambazo Ikulu ya Washington inasema zilikuwa zimebeba dawa za kulevya kutoka Venezuela. Alipoulizwa iwapo mashambulizi hayo yanaweza pia kulenga ardhi ya Venezuela katika siku zijazo, Trump alijibu: “Sitaki kukuambia kwa undani.” Lakini alipendekeza kwamba mashambulizi ya nchi kavu ni mojawapo ya machaguo ya serikali ya Washington.. Rais wa Marekani pia alithibitisha kwamba ameidhinisha Shirika la Ujasusi la Marekani (CIA) kufanya harakati nchini Venezuela.
Onyo la nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) na taasisi za kimataifa linaangazia ukiukaji kadhaa wa kimsingi wa sheria za kimataifa unaofanywa na Marekani, hasa katika muktadha wa mashambulizi dhidi ya meli za Venezuela katika Bahari ya Karibi:
Kwanza ni ukiukaji wa mamlaka ya kitaifa ya Venezuela: Operesheni yoyote ya kijeshi kwenye ardhi au eneo la maji ya nchi huru bila idhini kutoka kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa inatambuliwa kuwa ni ukiukaji wa wazi wa sheria za kimataifa na Mkataba wa jumuiya hiyo. Kupanga operesheni ndani ya Venezuela au kuidhinisha CIA kufanya “harakati za siri” nchini humo kunatathminiwa katika muktadhaa huo na ni kitendo cha uchokozi.
Pili ni utumiaji usio na uwiano wa nguvu ya mauaji: Chini ya sheria ya kimataifa, matumizi ya nguvu hatari yanaruhusiwa tu wakati kuna tishio la karibu kwa vikosi vya jeshi. Hata hivyo ripoti zinaonyesha kuwa katika mojawapo ya oparesheni hizo, meli iliyolengwa na Marekani ilikuwa ikigeuka na kurudi na haikuwa tishio kwa majeshi ya Marekani.
Tatu ni jaribio la kuhalalisha uhalifu. Ili kuhalalisha vitendo vyake, utawala wa Trump umetangaza kwamba Marekani iko katika “mapigano ya silaha” na wauza madawa ya kulevya wa “makundi yasiyo ya serikali.” Madai haya yanatokana na tafsiri yenye utata ya sheria za kimataifa ambayo imekosolewa vikali na wataalamu wa sheria.

Kuhusu malengo ya vitisho vya kijeshi vya Marekani dhidi ya Venezuela, tunaweza kuashiria yafuatayo:
Kwanza ni kutaka kudhibiti rasilimali za nishati: Venezuela ina akiba kubwa zaidi ya mafuta inayojulikana duniani. Wachambuzi na maafisa wengi wa Venezuela wanaamini kwamba lengo kuu la Marekani ni kutaka kudhibiti utajiri huu wa asili.
Pili ni utekelezaji wa Mwongozo wa Monroe: Mgogoro huu unaashiria kurejeshwa kwa sera ambayo inaitambua Marekani kuwa na haki ya kusimamia na kuingilia kati masuala ya nusu ya Magharibi mwa dunia. Mwelekeo huu una historia ndefu katika eneo la Amerika Kusini na daima umekuwa ukikabiliwa na upinzani kutoka kwa nchi za eneo hilo.
Tatu ni kupotosha maoni ya umma. Baadhi ya wachambuzi wa masuala ya ndani nchini Marekani wanaamini kwamba, uanzishaji huu wa mgogoro unaweza kugeuza mazingatio ya umma ya kuyaweka mbali na masuala ya ndani yenye utata nchini Marekani.
Hatimaye, inatupasa kusema kwamba, onyo la Jumuiya ya Nchi Zisizofungamana na Siasa za Upande Wowote (NAM) kuhusu uwezekano wa mashambulizi ya Marekani dhidi ya Venezuela si la kimaadili na kisiasa tu, bali ni onyo linalozingatia kanuni na sheria za kimataifa na ufahamu sahihi wa matokeo mabaya ya vita vipya. Mgogoro huo hautaishia Venezuela, bali pia utatoa changamoto kwa uhuru, usalama na kujitawala kwa nchi zote zinazoendelea.