Maswa. Wakulima wa zao la pamba wilayani Maswa, mkoani Simiyu, wamekabidhiwa matrekta 50 yaliyotolewa na Serikali kupitia Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), kwa lengo la kurahisisha shughuli za kilimo bora na kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.

Akizungumza leo Jumapili Oktoba 19, 2025, katika Kijiji cha Hinduki wilayani humo wakati wa hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney amesema Serikali imeamua kuwasaidia wakulima wa pamba kwa dhati ili kuongeza uzalishaji wa zao hilo ambalo ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini.

Dk Anney amesema matrekta hayo ya kisasa yatachochea mageuzi ya kilimo katika wilaya hiyo kwa kuwaondoa wakulima kwenye matumizi ya jembe la mkono na kuwawezesha kwenda sambamba na teknolojia ya kisasa ya kilimo chenye tija.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Anney akisisitiza jambo kwa madereva wa matrekta yaliyotolewa na serikali kwa ajili ya kuwalimia kwa bei nafuu wakulima wa zao la pamba katika wilaya hiyo.Picha na Samwel Mwanga

“Serikali imetoa matrekta haya ili mkulima wa kawaida aweze kulimiwa kwa gharama nafuu ya Sh35,000 kwa ekari moja. Tunataka kuona matrekta haya yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa, si kwa biashara binafsi wala kwa kuhujumu wakulima,” amesema.

Aidha, ametoa onyo kali kwa madereva na maafisa watakaohusika na uendeshaji wa matrekta hayo kuepuka vitendo vya wizi na hujuma ikiwemo kuuza vipuri kwa watu binafsi, akisisitiza kuwa hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaobainika.

“Madereva wazembe, walevi, wezi na wahujumu hawatapewa nafasi ya kuwalimia wakulima. Matrekta haya ni mali ya wananchi, hivyo yatumiwe kwa uadilifu na kwa manufaa ya wakulima,” amesisitiza Dk Anney.

Kwa upande wake, Mkaguzi wa Bodi ya Pamba Wilaya ya Maswa, Ally Mabrouk amesema msimu wa kilimo cha pamba wa mwaka 2025/2026 umeanza rasmi, na matrekta hayo ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha wakulima wanalimiwa kwa wakati na kwa gharama nafuu.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Anney akiwasha moja ya trekta yaliyotolewa na serikali kwa wakulima wa zao la pamba wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga

“Lengo letu ni kumuhudumia mkulima. Haya matrekta yameletwa ili kuondoa changamoto ya ukosefu wa zana za kisasa za kilimo. Tunataka kuona mashamba yote yanaingizwa kwenye uzalishaji mapema,” amesema Mabrouk.

Baadhi ya wakulima waliohudhuria hafla hiyo walieleza furaha yao kwa hatua hiyo ya Serikali, wakisema ni mara chache kuona juhudi za maendeleo zikiwa na matokeo ya moja kwa moja kwa mkulima wa chini.

Mariam Magesa, mkulima kutoka kijiji cha Hinduki amesema matrekta hayo yatawapunguzia gharama kubwa walizokuwa wakitumia kulimia kwa kutumia wanyama au kukodi matrekta binafsi kwa bei ya juu.

Mkuu wa wilaya ya Maswa,Dk Vicent Anney (mwenye kofia)akiwasha moja ya trekta yaliyotolewa na serikali kwa wakulima wa zao la pamba wilayani humo.Picha na Samwel Mwanga

“Tulikuwa tunalipa hadi Sh70,000 kwa ekari moja kwa matrekta binafsi, lakini sasa bei imeshuka hadi nusu yake. Hii ni faraja kubwa kwetu wakulima,” amesema.

Naye Kisandu Khija, mkulima wa kijiji cha Isageghe amesema changamoto kubwa imekuwa ucheleweshaji wa matrekta mashambani na ubovu wa baadhi ya zana hizo, akaiomba bodi kuhakikisha zinapata matengenezo kwa wakati.

“Tunaiomba bodi ihakikishe matrekta haya yanahudumiwa ipasavyo. Tukichelewa kulima, tunapoteza msimu mzima,” amesema.

Utoaji wa matrekta hayo ni sehemu ya mpango wa serikali kupitia TCB wa kuhakikisha wakulima wa pamba wanapata zana bora za kisasa ili kuongeza uzalishaji na ubora wa pamba inayozalishwa nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *