Simba ipo ugenini katika Uwanja wa Somhololo leo huko Eswatini ambako kuanzia saa 10:00 jioni kwa muda wa Tanzania, itakabiliana na wenyeji wao, Nsingizini Hotspurs katika mechi ya raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.

Ushindi katika mchezo huo utaifanya Simba ijiweke katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya makundi ya mashindano hayo.

Wakati mchezo huo ukibakiza saa chache kabla ya kuanza, Simba itaingia uwanjani ikiwa na historia nzuri ya ubabe nchini Eswatini.

Kumbukumbu zinaonyesha Simba haijawahi kupoteza mechi katika ardhi ya Eswatini mara zote ilizoenda kucheza mechi za mashindano ya klabu Afrika lakini pia haijawahi kutolewa na timu ya Eswatini mara tatu tofauti ambazo ilipangwa kukutana nazo.

Mwaka 1977, Simba ilipangwa kukutana na Mbabane Highlanders katika raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa na ikasonga mbele baada ya timu hiyo ya Eswatini kujitoa mashindano.

Mwaka 1993, Wawakilishi hao wa Tanzania walipangwa kukutana na Manzini Wanderers ya Eswatini katika raundi ya pili ya Kombe la CAF na Simba ikasonga mbele kwa ushindi wa mabao 2-0 ambapo ilishinda bao 1-0 katika kila mechi nyumbani na ugenini.

Msimu wa 2018/2019, Simba ilipangwa kukutana na Mbabane Swallows ya Eswatini katika raundi ya awali ya Ligi ya Mabingwa Afrika na ikasonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 8-1.

Katika mchezo wa kwanza nyumbani Dar es Salaam, Simba iliibuka na ushindi wa mabao 4-1 na ikaenda kushinda mabao 4-0 ugenini huko Eswatini.

Katika mchezo wa leo, wawakilishi hao wa Tanzania watawakosa Mohamed Bajaber ambaye bado hajawa fiti baada ya kupona majeraha lakini pia watamkosa kipa Mousa Camara ambaye ni majeruhi.

Meneja Mkuu wa Simba, Dimitar Pantev amesema kuwa kikosi chake kipo kamili kwa ajili ya mchezo huo.

“Maandalizi yako kawaida, ingawa kidogo tofauti kwa sababu tunatumia uwanja wenye nyasi bandia. Lakini timu iko tayari, imepata motisha ya kutosha na nafikiri lengo letu ni kutoa uwezo wetu wote, kucheza vizuri na kama nilivyosema awali, kila kitu kitategemea utendaji wetu. Hivyo tutafuata mbinu yetu tuliyojiandaa nayo.

“Hatutabadilisha chochote. Tuna mtindo wetu wa kucheza na tutacheza soka letu. Nafikiri kila kitu kitaenda sawa kwetu. Labda itakuwa ngumu kidogo kwa wachezaji wetu kwa sababu hapa kuna baridi sana, lakini huu ni mchezo wa mpira wa miguu, hali ni ile ile kwa sisi na kwa wao pia,” amesema Pantev.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *