Mbeya. Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya (MNEC), Ndele Mwaselela, amezindua kampeni maalumu iitwayo; “Amka Twende Pamoja Kupiga Kura,” yenye lengo la kuhamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kushiriki kupiga kura Oktoba 29 mwaka huu.

Uzinduzi huo umefanyika katika mwendelezo wa ziara yake ya kukutana na makundi mbalimbali katika wilaya za Mkoa wa Mbeya, ambapo ananadi sera za CCM na kuwaombea kura madiwani, wabunge na mgombea urais wa chama hicho, Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza wilayani Kyela, Mwaselela amesema dhamira ya ziara hiyo ni kutoa elimu ya mpiga kura na kuhamasisha wananchi kutumia haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kwa wingi siku ya uchaguzi.

“Kampeni ya ‘Amka Twende Pamoja Kupiga Kura’ inalenga kuhakikisha kila mwananchi anahamasika kutoka na mwenzake siku ya Oktoba 29, ili wote watimize wajibu wao wa kikatiba kuchagua viongozi, hususan wa Chama Cha Mapinduzi,” amesema Mwaselela.

MNEC huyo ambaye pia ni Kaimu Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mbeya, ameeleza kuridhishwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika maeneo aliyotembelea, akibainisha kuwa ziara yake itakamilika Oktoba 28 baada ya kufika katika wilaya zote za mkoa huo.

“Kama mdau wa uchaguzi, jukumu langu ni kutoa msukumo kwa wananchi kujitokeza kupiga kura. Hadi sasa nimeridhishwa na mwitikio wao, na ifikapo Oktoba 28 nitakuwa nimehitimisha ziara yangu katika wilaya zote,” amesema.

Kwa upande wake, kada wa CCM, Denis Jerome, amesema chama hicho kina dhamira ya kushinda nafasi zote kutokana na kukubalika kwake kwa wananchi kupitia sera na hoja madhubuti.

“Tunampongeza MNEC wetu kwa kazi kubwa ya kujitolea kutangaza chama na kuwanadi wagombea. Rais Samia amefanya mambo makubwa, na Oktoba 29 kazi ni moja tu, kutiki CCM,” amesema Jerome.

Naye Catherine Novath, akizungumza kwa niaba ya vijana, amesema kundi hilo lina wajibu wa kutimiza haki yao ya kikatiba kwa kujitokeza kupiga kura, akisisitiza kuwa CCM kinaendelea kuaminiwa na wananchi.

“Wagombea wa CCM wanazo sifa zote. Kazi yetu sisi vijana ni kujitokeza kwa wingi kupiga kura na kutopelekwa na maneno ya mitandaoni. Tuna imani CCM itashinda,” amesema Catherine.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *