London, England. Dakika 18 baada ya kupoteza kwa mabao 3-0 dhidi ya Chelsea katika mechi ya Ligi Kuu England iliyopigwa jana, Jumamosi Oktoba 18, 2025, Nottingham Forest iliamua kumfukuza kazi kocha wake, Ange Postecoglou.

Postecoglu ambaye amewahi kuwa kocha wa Tottenham Hotspur amepoteza michezo sita kati ya nane aliyosimamia katika kipindi chake cha siku 39 kama kocha wa Forest huku akiwa hajapata ushindi wowote akitoa sare mechi mbili.

Kwa mujibu wa taarifa, tajiri na  mmiliki wa timu hiyo, Evangelos Marinakis alifanya uamuzi wa kumfukuza Postecoglou dakika 18 tu baada ya mechi kumalizika.

“Klabu ya Nottingham Forest inapenda kuthibitisha kuwa, baada ya mfululizo wa matokeo ya kiwango kisichoridhisha, Ange Postecoglou ameondolewa majukumu yake kama kocha mkuu kuanzia sasa. Klabu haitatoa taarifa zaidi kwa wakati huu.”

Ripoti za awali zinawataja makocha kama Sean Dyche na Marco Silva wa Fulham wanaweza kupewa mikoba ya kuinoa timu hiyo.

Postecoglou alijiunga na Forest Septemba 9, 2025 kuchukua nafasi ya Nuno Espirito Santo, baada ya kufukuzwa kazi Tottenham licha ya kuiwezesha kushimda taji la Europa League msimu uliopita. Amedumu ndani ya kikosi hicho kwa takribani siku 39.

Hata hivyo, mambo hayakwenda vizuri akipoteza mechi sita kati ya nane, huku nyingine mbili zikiisha kwa sare.

Kocha huyo wa zamani wa Celtic, pia alikuwa akizomewa sana na mashabiki wa timu hiyo katika mechi za hivi karibuni kutokana na matokeo mabovu.

Kipigo cha mabao 3–2 dhidi ya Midtjylland katika Europa League kilimfanya kuwa kocha wa kwanza wa Forest kushindwa kushinda mechi zake sita za kwanza baada ya miaka 100.

Licha ya yote, Postecoglou alisisitiza kuwa angeweza kugeuza hali hiyo lakini hilo halijaonekana kufanikiwa na badala yake amepewa mkono wa kwaheri.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *