
Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (HAMAS) imekanusha vikali madai yaliyomo katika taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani kwamba harakati hiyo imekiuka makubaliano ya kusitisha mapigano huko Gaza.
Hamas imesema: Madai ya “kukaribia mashambulizi” au “ukiukwaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano” ni ya uongo na yanaendana kikamilifu na propaganda za kupotosha za Israel, zinazotoa kifuniko na mwavuli wa kuhalalisha uhalifu, uvamizi na uchokozi unaoendelea kufanywa na utawala ghasibu dhidi ya watu wetu.
Wakati huo Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) ilisema jana Jumamosi kwamba, uamuzi wa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, wa kuzuia kufunguliwa kivuko cha Rafah hadi ilani nyingine ni ukiukaji wa wazi wa masharti ya makubaliano ya usitishaji vita na kukiuka ahadi alizotoa kwa wapatanishi na wadhamini wa makubaliano hayo.
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu alisema kuwa kivuko cha mpaka cha Rafah kati ya Ukanda wa Gaza na Misri kitaendelea kufungwa hadi litakapotolewa tangazo jingine, na kwamba kufunguliwa kwake kutategemea Hamas kukabidhi miili ya wateka wa Israel.
Matamshi ya Netanyahu yamekuja baada ya ubalozi wa Palestina mjini Cairo kutangaza kufungua tena kivuko cha Rafah kuanzia Jumatatu “ili kuwawezesha raia wa Palestina wanaoishi katika Jamhuri ya Kiarabu ya Misri wanaotaka kurejea Ukanda wa Gaza.”