
Jenerali Abdel-Fattah al Burhan, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan amesema jeshi la nchi hiyo liko tayari kwa mazungumzo ya “kumaliza vita na kurejesha umoja na heshima ya nchi hiyo.”
Akizungumza huko Atbara, kaskazini mwa Sudan huku akitoa mkono wa pole wa familia ya Muzammil Abdullah, afisa wa jeshi aliyeuawa hivi karibuni katika mapigano huko al Fasher, Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan amesema kuwa hakuna mazungumzo yanayoendelea hivi sasa kati ya Sudan na Marekani, Saudi Arabia, Misri na Imarati au upande mwingine wowote.
Burhan amesisitiza kuwa vikosi vya ulinzi vya nchi hiyo vitaendelea kukabiliana na adui.
Jenerali Abdel-Fattah al Burhan amesema kuwa Sudan inawakaribisha wale wote wenye nia ya kweli kuhakikisha kuwa amani inarejeshwa nchini.
Mkuu wa Baraza la Utawala wa Sudan ameeleza haya kabla ya kufanyika mkutano mjini New York ambao umepangwa ili kutafuta ufumbuzi wa amani kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Jeshi la Sudan na wanagambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) wamekuwa wakipigana tangu mwezi Aprili mwaka 2023; vita ambavyo hadi sasa vimeuwa watu zaidi ya 20,000 na kusababisha wengine milioni 14 kuwa wakimbizi.
Muungano wa Waasisi wa Sudan, unaoongozwa na wanamgambo wa kikosi cha RSF mwezi Julai ulitangaza kuundwa kwa serikali sambamba inayoongozwa na kiongozi wa RSF Mohamed Hamdan Dagalo. Serikali ya Sudan ililaani vikali hatua hiyo.