Chama tawala nchini Zimbabwe cha ZANU-PF kimesema kitaanzisha taratibu za kurefusha muhula wa Rais Emmerson Mnangagwa kwa miaka miwili zaidi, na hivyo kumfanya aendelee kukaa madarakani hadi 2030.

Pendekezo hilo liliidhinishwa jana Jumamosi wakati wa kongamano la kila mwaka la chama hicho katika mji wa mashariki wa Mutare, ambapo wajumbe waliiagiza serikali kuanza kuandaa sheria ya kurekebisha Katiba, kwa mujibu wa Waziri wa Sheria na Masuala ya Kisheria wa chama hicho, Ziyambi Ziyambi.

Wataalamu wa sheria wanasema Katiba inamtaka Mnangagwa, 83, kuondoka madarakani mwaka 2028 baada ya kukamilisha mihula miwili, na marekebisho yoyote yatahitaji marekebisho ya Katiba na pengine kura ya maoni.

Kupitishwa kwa pendekezo hilo kulipokelewa kwa nderemo na vifijo kutoka kwa wajumbe, jambo lililoakisi mtindo wa uongozi wa chama hicho tangu uhuru wa nchi hiyo mwaka 1980.

Chama cha ZANU-PF kinadhibiti Bunge, suala ambalo linakipatia ushawishi mkubwa, licha ya maonyo yanayotolewa kuhusu changamoto za kisheria zinazoweza kupinga hatua hiyo.

Hapo awali Mnangagwa alisisitiza kuwa ataheshimu Katiba na kwamba hana nia ya kubakia madarakani baada ya muhula wake kkumalizika. Hata hivyo, wafuasi wake wameshinikiza kimya kimya kuongezwa kwa muhula wake tangu uchaguzi wa mwaka jana uliokumbwa na utata. Mwelekeo huu unapingwa na mrengo wenye uhusiano na Makamu wa Rais, Constantino Chiwenga ndani ya chama tawala cha ZANU-PF.

Mnangagwa aliingia madarakani mwaka 2017 baada ya kumwondoa madarakani aliyekuwa Rais wa Zimbabwe, Robert Mugabe, akiahidi mageuzi ya kidemokrasia na kiuchumi. Hata hivyo, wapinzani wake wanamshutumu kuwa amegeuza uchaguzi kuwa wa kimaonyesho tu, kudhoofisha Mahakama, na kukandamiza upinzani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *