
Chanzo cha picha, Getty Images
Baada ya mkutano wa 12 wa kilele wa Jumuiya ya Nchi za Turkic, uliofanyika katika mji wa Kibla, Azerbaijan, vyombo vya habari vinavyounga mkono Kremlin na wachambuzi walieleza wasiwasi wao kuhusu mipango ya ushirikiano wa kijeshi yaliyopendekezwa katika mkutano huo, huku baadhi wakieleza shirika hilo kuwa ni kambi ya kijeshi inayoibuka, chini ya ushawishi wa Uturuki.
Nchi za Turkic ni Azerbaijan, Kazakhstan, Kyrgyzstan, Türkiye, na Uzbekistan, ambazo ni wanachama kamili wa Jumuiya ya Nchi za Turkic (OTS). Nchi nyingine za Turkic, kama vile Turkmenistan, ni mataifa waangalizi, pamoja na Hungaria na Jamhuri ya Uturuki ya Cyprus ya Kaskazini (TRNC).
Kwa mujibu wa tovuti binafsi ya habari ya Orda, Rais wa Azerbaijan Ilham Aliyev, ambaye anashikilia urais wa zamu na jumuiya hiyo, amependekeza kufanyika mazoezi ya pamoja ya kijeshi ya nchi wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Turkic kwenye Jamhuri ya Azerbaijan mwaka 2026.
Katika hotuba yake, Aliyev alitolea mfano wa uzoefu mkubwa wa Jamhuri ya Azerbaijan katika kufanya mazoezi zaidi ya 25 ya kijeshi na Uturuki mwaka jana.
Arkady Dubnov, mchambuzi wa siasa, aliiambia tovuti hiyo kwamba pendekezo hilo linaonyesha nia ya Azerbaijan ya kuonyesha nguvu zake za kijeshi katika eneo hilo baada ya ushindi wake dhidi ya Armenia.
“Inaonekana jeshi la Jamhuri ya Azerbaijan sasa ni jeshi la pili kwa nguvu katika kanda hiyo baada ya Uturuki, lakini muhimu zaidi, lina uzoefu halisi na vita,” alisema.
Lakini Dubnov aliondoa uwezekano wa muungano huo kugeuka kuwa kambi ya kijeshi na kisiasa kama Shirika la Mkataba wa Usalama wa Pamoja linaloongozwa na Urusi. Amesema, “haya ni matarajio yaliyopitiliza na matamanio yasiyowezekana.”
Wachambuzi wa Urusi

Chanzo cha picha, Getty Images
Idhaa ya uchambuzi ya Vesti Express 24 inayounga mkono serikali ya Urusi, imeelezea kuwa udhaifu wa kiuchumi” wa wanachama wa Jumuiya ya Nchi za Turkic, unadhoofisha mipango ya jumuiya hiyo, kwani biashara za nchi wanachama zinachangia “asilimia 7 tu ya mauzo yao yote ya biashara ya nje.”
Tovuti inayounga mkono Kremlin PolitNavigator ilielezea ziara ya Rais wa Urusi Vladimir Putin nchini Tajikistan kama jaribio la kukabiliana na “kuundwa kwa kambi ya kijeshi na kisiasa ya mataifa ya Turkic, ambayo itaungwa mkono na Türkiye na NATO.”
Tovuti hiyo imeandika: “Dushanbe [mji mkuu wa Tajikistan] ni mji muhimu kwa Urusi kufuatilia mabadiliko katika eneo hilo, wakati Jumuiya ya Mataifa ya Turkic yakibadilika na kuwa kambi ya kijeshi na kisiasa chini ya bendera za Uturuki na NATO.”
PolitNavigator inaichukulia Tajikistan kuwa mshirika pekee wa Urusi ambaye hana ushirika na Uturuki katika Asia ya Kati, na wameingia makubaliano ya nchi hizo mbili ya kuimarisha kambi ya kijeshi ya 201 ya Urusi na kuzuia “kuingiliwa na nchi na mashirika yasiyofungamana na ushirka wao.”
Chombo hicho kinasema: “Lengo haswa ni kukabiliana na jeshi ambalo ni wakala wa NATO, ambalo litajifanya kuwa ‘Muungano wa Turkic na, likiongozwa na London na Washington, na kupelekea kudhoofisha eneo hilo.”
Igor Shestakov, mkurugenzi wa Kituo wa Ovi Ordo, kupitia chaneli ya Telegram, inayounga mkono Kremlin, Asiatsky Express, ameuita mkutano huo kuwa ni “mabadiliko ambapo ajenda ya kiuchumi imegeuka kuwa ajenda ya kiitikadi.”
Ameonya kwamba mipango inayohusiana na ushirikiano wa kijeshi, ikiwa ni pamoja na mkutano wa 2025 wa makatibu wa Baraza la Usalama huko Bishkek na pendekezo la Uzbekistan la kufanya mikutano ya kijasusi ya mara kwa mara huko Samarkand, ni ishara ya kuundwa kwa kambi hiyo.”
“Kwa maoni yangu, matarajio ya kuunda Jeshi la Pamoja inakaribia hatua kwa hatua,” Shestakov aliandika. “Mazoezi ya pamoja yaliyopangwa na Jamhuri ya Azerbaijan kwa 2026 ni uthibitisho kwamba njia ya kuunda kambi ya kijeshi inazidi kuwa ya wazi kila siku.”