Mbeya. Mgombea udiwani wa Chama cha Wananchi (CUF) Kata ya Itezi, Erasto Juma ameonesha kusikitishwa na changamoto ya upatikanaji wa maji katika Mtaa wa Gombe, akiahidi kuwa iwapo atachaguliwa, kero hiyo itabaki historia.
Akizungumza leo Jumapili, Oktoba 19, 2025, Juma amesema muda wa mabadiliko umefika na njia bora ya kupata maendeleo ni kwa wananchi wa Itezi kukichagua Chama CUF.
“Waliochimba visima wanastahili pongezi na tuwaombee, kwani wameisaidia jamii kukabiliana na changamoto ya maji licha ya kulipia huduma kwa Sh100. Nipeni kura nimalize tatizo hili la maji, haiwezekani kuendelea kuishi kwa hofu ya magonjwa,” amesema Juma.
Amesema endapo atashinda, ataratibu mkutano wa hadhara ndani ya siku 60 hadi 90 kueleza utekelezaji wa ahadi zake kwa wananchi, huku akiwataka kufanya uamuzi wa busara kumpa nafasi ya Udiwani.
Amesisitiza kuwa hatakuwa kiongozi wa kujitenga na wananchi, bali atawapa mawasiliano yake binafsi ili waweze kumfikia moja kwa moja pindi wanapohitaji msaada, bila kujali tofauti za vyama, dini au kabila.
Mbali na kero ya maji, Juma ameahidi kuboresha miundombinu ya barabara kwa kujenga miferejinakufuta michango ya shule za msingi, hususan kwa wanafunzi wa darasa la nne.
“Michango kama ya mitihani na taaluma nitaipeleka hoja Halmashauri ili ifutwe. Iwapo itashindikana, nitahakikisha inapitiwa upya kwa sababu nimejitoa kwa ajili ya wananchi wa Itezi,” amesema Juma.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CUF Mbeya Mjini, Yassin Mrotwa amesema chama hicho kina kila sababu ya kushinda katika ngazi zote za uongozi, kwa kuwa wananchi wamechoshwa na utawala wa chama kimoja kwa muda mrefu.

Ametaja baadhi ya mambo yanayowakandamiza wananchi kuwa ni pamoja na bei kubwa ya mafuta na sukari ikilinganishwa na nchi jirani kama Malawi.
“Malawi mafuta ni Sh1,950 na sukari Sh2,400. Tujiulize hapa kwetu hali ikoje? Oktoba 29 ni siku ya kufanya mabadiliko. Wagombea wetu wana sifa, tuwape kura waongoze,” amesema Mrotwa.
Katika mkutano huo uliofanyika Mtaa wa Gombe,Mgombea Ubunge wa DP Jimbo la Mbeya Mjini, Telespho Joseph, amehimiza wananchi kuwachagua wagombea wa CUF katika nafasi za Udiwani na Ubunge wa Uyole, akisema ni watu waadilifu na wachapakazi.
“Mnayo bahati kubwa ya kuwa na wagombea wenye nia njema na uwezo. Nimeamua kuwasapoti kwa dhati, wapeni kura wakaongoze,” amesema Joseph.
Naye Mgombea Ubunge wa CUF Jimbo la Uyole, Ibrahim Mwakwama, amesema kipaumbele chake kikuu ni kutumia fedha za Mfuko wa Jimbo kulipia michango ya shule kwa wanafunzi, akieleza kuwa sera ya elimu bure bado haijatekelezwa ipasavyo.
“Wanafunzi wa shule za serikali wanabeba madaftari 10, wakati wa shule binafsi wanabeba kati ya mawili hadi manne. Hii inamaanisha wa shule za serikali wanaandaliwa kubeba mizigo, wengine kuwa watawala. Nitapambana kuweka usawa,” amesema Mwakwama.
Ameongeza kuwa kabla ya kugombea ubunge, aliwahi kupigania ujenzi wa ofisi ya kata na zahanati, hivyo ana uzoefu wa kutatua changamoto za wananchi.
“Kama unajenga barabara halafu watu wanatekwa na kupotezwa, maendeleo hayo hayana maana. Nikipewa nafasi bungeni nitashughulikia usalama, kuunganisha wananchi na kuhakikisha elimu inawapa fursa sawa wote,” amesema Mgombea huyo.