Benki ya CRDB imeingia ubia wa kimkakati wenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 300 na taasisi tatu za kimataifa ili kukuza ujasiriamali, kuimarisha biashara na kuboresha makazi katika mataifa ya Afrika Mashariki na Kati.
Mikataba hiyo imesainiwa katika Jukwaa la Wabia na Wawekezaji lililofanyika kando ya Mikutano ya Mwaka ya Benki ya Dunia na IMF jijini Washington, Marekani, ikihusisha FinDev Canada, DEG (KfW Group) ya Ujerumani, na Shelter Afrique Development Bank.
Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB, Abdulmajid Nsekela, amesema FinDev Canada imewekeza dola milioni 60 (shilingi bilioni 150) kusaidia miradi ya wajasiriamali, hasa wanawake na vijana, na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. DEG imewekeza dola milioni 50 (shilingi bilioni 125) kuimarisha biashara ndogo na za kati na kuunda ajira kwa vijana, huku Shelter Afrique Development Bank ikichangia dola milioni 10 (shilingi bilioni 25) kwa makazi nafuu nchini DRC.
Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi wa serikali kutoka Tanzania, Burundi na DRC, wakiwemo mawaziri na magavana wa Benki Kuu, pamoja na mabalozi wa Tanzania na Burundi nchini Marekani.
✍ @claud_jm
#AzamTVUpdates