Tarehe 31 mwezi Oktoba mwaka 2000, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilipitisha Azimio namba 1325 lililotambua madhara ya migogoro kwa wanawake na wasichana, na kuthibitisha haki yao ya kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa amani. Azimio hilo ndilo ambalo limeanzisha ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama (WPS) – likilenga kuwawezesha wanawake duniani kote kujenga na kudumisha amani endelevu.

Lakini je, malengo haya makubwa ya kimataifa yanafika vipi kwa wanawake wanaoishi vijijini, kwenye kambi za wakimbizi au maeneo yenye migogoro?

Shirika la Umoja wa Mataifa la Masuala ya Wanawake (UN Women) imezungumza na wanawake nchini Uganda wanaoonesha jinsi amani inavyoweza kuchipua kwenye jamii, kwa juhudi za watu wanaoelewa changamoto za eneo lao na wanaoshirikiana kutafuta suluhu.

Wanawake wenye uzoefu wa moja kwa moja wanaongoza ujenzi wa amani

Usingejenga njia ya walemavu bila kumshirikisha mtu anayetumia hiyo njia kwa kutumia kiti mwendo,” amesema Juliet Mbambu, Mkurugenzi wa Chama cha Wanawake Wenye Ulemavu wa Bwera “Usipowaelewa wale unaowasaidia, unaweza kuwajengea mlima badala ya njia rahisi. Kauli yetu ni ‘Hakuna kitu kwa ajili yetu bila sisi.’”

Mbambu, aliyepooza kutokana na ugonjwa wa polio akiwa na umri wa miaka 10, sasa ni mfanyakazi wa kijamii na mama wa watoto watatu. Ameunda vikundi vya kusaidia watoto wenye ulemavu na wazazi wao, akilenga kuelimisha jamii na kutetea haki zao.

Akiimarishwa na mafunzo ya usuluhishi wa migogoro aliyopokea kupitia Muungano wa Utekelezaji wa Azimio namba 1325 (CoACT) kwa msaada wa UN Women, Juliet anaongoza midahalo ya kijamii kuzuia misimamo mikali na kuwafikia vijana wanaolengwa na makundi ya kigaidi. “Mwisho wa mazungumzo, vijana wenyewe huibuka na mikakati ya kupambana na msimamo mkali na kuwaelimisha wenzao,” amesema.

Angel Musiime, afisa wa kata na mpatanishi wa amani katika wilaya ya Kyegegwa iliyopo magharibi mwa Uganda

UN Women/Solomon Tumwesigye

Angel Musiime, afisa wa kata na mpatanishi wa amani katika wilaya ya Kyegegwa iliyopo magharibi mwa Uganda

Kuwezesha vijana kunachochea amani

Kwa Angel Musiime, afisa wa kata na mpatanishi wa amani katika wilaya ya Kyegegwa iliyopo magharibi mwa Uganda, kazi yake ni wito wa moyo. Ameshawahi kuwashauri wavulana kurejea shuleni na kuwasaidia wanawake walioko kwenye ndoa zenye mateso.

Nataka kuwa mwanamke kinara katika kuleta amani,” amesema Angel mwenye umri wa miaka 26.

Imembidi kushinda vikwazo vyake mwenyewe kama mwanamke kijana, ikiwa ni pamoja na kumpoteza mama yake na kupata ujauzito bado akiwa chuo kikuu. Angel anakumbuka jamii ikimwambia “maisha yako yameisha.” Lakini hakukata tamaa. “Sauti ndani yangu iliniambia, ‘Mfanye mama yako ajivunie.’”

Mwaka 2023, akapata nafasi kuhudhuria mafunzo ya wapatanishi wa amani na CoACT. “Nilijua sasa ninaweza kutetea wanawake na wasichana kupata haki sawa,” amesema huku akitabasamu. “Kupitia ujuzi huo, nimeweza kugusa maisha ya watu wengi.”

Ujenzi wa amani unahitaji kukutana na watu moja kwa moja

Sharon Kabugho, Afisa Mawasiliano wa Serikali ya Wilaya ya Kasese iliyopo magharibi mwa Uganda karibu na mpakani mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), kwake kazi ya ujenzi wa amani inamaanisha kujitolea bila kikomo. “Kama hakuna nafasi kwenye gari, napanda nyuma ya pick-up. Lazima nifike,” amesema akicheka.

Kupitia Mpango wa Tatu wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, Uganda inalenga kuzuia migogoro kuanzia ngazi ya chini, ikiwemo migogoro ya ardhi na ukatili wa kijinsia.

Kabugho amesema mafanikio yanategemea kuwafikia wadau wote — viongozi wa dini, mila na serikali za mitaa — na kuwasaidia kuelewa maana halisi ya amani. “Amani ni kuona utu wa mtu mwingine, na kutambua wanawake ni sawa kama watu wengine.”

Anatumia redio, mitandao ya kijamii na simu za dharura kuwasaidia wanawake wanaokabiliwa na ukatili. “Kwa ajili ya amani, na kwa sababu wanawake bado wanateseka, lazima tuendelee. Kila mmoja anapaswa kushiriki kuhakikisha ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama inatekelezwa,” amesema.

Sharon Kabugho, Afisa Mawasiliano wa Serikali ya Wilaya ya Kasese iliyopo magharibi mwa Uganda.

UN Women/Solomon Tumwesigye

Sharon Kabugho, Afisa Mawasiliano wa Serikali ya Wilaya ya Kasese iliyopo magharibi mwa Uganda.

Wanawake ni nguzo ya amani endelevu Uganda

Jamii inayohakikisha usalama wa wanawake, inahakikisha utulivu wake pia,” amesema Adekemi Ndieli, Naibu Mwakilishi wa UN Women nchini Uganda.

Kwa ufadhili wa Serikali ya Norway, UN Women imewezesha uundaji wa Mipango 16 ya Utekelezaji ya Kijamii. Uwakilishi wa wanawake kwenye kamati za amani umeongezeka kutoka asilimia 17 mwaka 2022 hadi asilimia 46 mwaka 2025.

Mwaka 2024 pekee, takribani migogoro 500 katika ngazi ya jamii ilisuluhishwa kwa mafanikio na wanawake tunaofanya nao kazi,” amebainisha Ndieli. “Wanawake, wanaume na vijana sasa wanashiriki kikamilifu katika shughuli za amani, ulinzi na kuboresha maisha yao.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *