
Chanzo cha picha, Ikulu Ya Rais
-
- Author, Asha Juma
- Nafasi, BBC Nairobi
Kwa miaka mingi unapozungumzia siasa za Kenya, huwezi kumuacha nje Waziri Mkuu wa zamani Raila Amolo Odinga aliyeaga dunia nchini India Jumatano Oktoba 15 alipokuwa akipata matibabu.
Na asiye mgeni wa siasa utakubaliana nami kwamba hakuna adui wala rafiki wa kudumu kwenye ulingo huu wa siasa.
Katika makala hii, tuangazia matukio ya kisiasa ambayo yalibadilisha uhusiano wa Raila Odinga na Rais William Ruto na kuwafanya kuonekana marafiki au mahasimu wakubwa machoni mwa wafuasi wao katika safari yao ya kisiasa ya takriban miongo mitatu.
Safari ya kisiasa ya Ruto na Odinga
Safari ya kisiasa ya William Ruto kwa kifupi tu unaweza kusema ilianzia mwaka 1992, alipojiunga na vugu vugu la vijana wa chama cha Kanu wakati huo ikijulikana kama Youth for Kanu 92 (YK’92) lililokuwa linaunga mkono kuchaguliwa kwa Rais Daniel Arap Moi katika uchaguzi wa mwaka 1992, uliokuwa mwanzo wa siasa za vyama vingi baada ya miaka zaidi ya 25 ya utawala wa KANU.
Mwaka huo, Raila Odinga alichaguliwa kuwa mbunge wa eneo la Lang’ata jijini Nairobi kupitia chama cha Ford Kenya.
Kipindi hiki hawakuwa na uhusiano wa karibu ila kila mmoja alikuwa akifanya kazi inayoonekana na wengi katika kambi yake.
Mwaka 1997, William Ruto alichaguliwa kwa mara ya kwanza kuwa mbunge wa Eldoret Kaskazini huku Raila Odinga akichaguliwa tena katika kiti cha ubunge wa Lang’ata lakini akiwa naye kwa mara ya kwanza amepoteza urais kupitia chama cha National Development Party (NDP). Na hapa ndipo walipopata fursa ya kutangamana hasa bungeni.
Miaka mitatu baadaye, Chama cha NDP kikatangaza kuungana na chama tawala cha KANU ambako Ruto alikuwa kiungo muhimu huko.
Mwaka 2001, Raila alichaguliwa kama Waziri wa Nishati huku Ruto akiwa Waziri msaidizi katika ofisi ya rais. Kupitia muungano huo, Raila Odinga alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha KANU.
Ikimbukwe kuwa siasa hizi za Raila zilianza baada ya kuwekwa kizuizini na Moi kwa miaka minane bila kufunguliwa mashtaka.
Hata hivyo, muda mfupi baadaye Raila na chama chake kwa ujumla waligundua njama za Rais Moi kutaka kumchagua Uhuru Kenyatta kama mrithi wake, wazo ambalo hawakukubaliana nalo na kuamua kuvunja muungano wao wa kisiasa.
Athari yake ni kwamba, Odinga aliondoka sio tu na wafuasi wake lakini hata na wafuasi wa KANU na kukiacha chama cha Rais Moi kikiwa kimepungua nguvu.
Hata hivyo, Ruto alisalia KANU na kuchaguliwa kuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi.
Ukweli ni kwamba hadi kufikia hapo, walikuwa wametangamana kikazi na bila shaka walikuwa wanajuana kwa kiasi fulani.
Mwaka 2002, Chama ambacho Ruto alikiunga mkono cha KANU kikapoteza huku cha Raila cha NDP kikiungana na muungano wa National Rainbow Coalition (Narc) ambacho mgombea wake alikuwa Mwai Kibaki kikipata ushindi.
Na wakati huu, Ruto akawa kwenye upinzani naye Raila akiwa kwenye serikali.
Raila na Odinga walipokuwa na maono yanayofanana

Chanzo cha picha, Raila Odinga/ Facebook
Siasa zikaendelea kama kawaida hadi mwaka 2005 walipounganishwa na harakati za kutafuta Katiba Mpya.
Kipindi hicho Ruto alikuwa Katibu Mkuu wa chama cha KANU, serikali ikapendekeza Katiba mpya.
Hapa, Raila na Ruto walishikana na kufanya kampeni za kupinga serikali iliyopendekeza Katiba mpya. Upande wa serikali ulioongozwa na Mwai Kibaki ulisema ‘Yes’ ukiashiriwa na alama ya ndizi huku upinzani uliopinga Katiba mpya ukisema ‘NO’ na kuashiriwa na alama ya chungwa.
Waliopinga walipata ushindi wa asilimia 58.12. Na kufuatia hili, Rais Mwai Kibaki alivunja Baraza lake lote la Mawaziri.
Wakati Kibaki alipowafuta kazi Raila na washirika wake, walishikana na kuunda chama cha ODM.
Ndoa ya kwanza ya kisiasa ya Raila na Ruto
Kipindi hiki, Ruto alikuwa mpinzani mwenye utata dhidi ya utawala wa Kibaki na baadaye, alitangaza kuondoka KANU na kujiunga na Orange Democratic Movement ODM.
Uhusiano wa kisiasa wa Raila na Ruto ilionekana kwenda vizuri hadi mwishoni mwa mwaka 2007 walipokwenda kwenye uchaguzi. Ruto alimuunga mkono Raila kwenye uchaguzi huo ambao ulikumbwa na utata. Matokeo yake yalipingwa vikali na upinzani na kusababisha na ghasia za baada ya uchaguzi.
Na mwisho wa siku, kukawa na “Timu ya upatanishi” mwaka 2008 ya jopo la Umoja wa Afrika ambalo lililoongozwa na Kofi Annan, kwa usaidizi wa viongozi kama Benjamin Mkapa na Graca Machel.
Kitumbua cha Raila na Ruto kilipoingia mchanga

Chanzo cha picha, Raila facebook
Kama sehemu ya utekelezaji wa mkataba wa maridhiano, Rais Mwai Kibaki alikaribisha upinzani na kuunda serikali ya umoja wa kitaifa Raila Odinga akiteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa Kenya kutoka 2008 hadi 2013, mwandani wake Wiliam Ruto akipata nafasi ya kuwa Waziri wa Kilimo kutoka 2008 hadi 2013, na Waziri wa Elimu ya Juu kutoka mwaka 2010 hadi 2011.
Matukio yaliyofuta baada ya hapo ndio yalifanya kitumbua cha Raila na Ruto kuanza kuingia mchanga.
Ruto aliwahi kusimulia kilichotokea katika moja wapo ya mikutano ya kisiasa, “Tulikubaliana kwa hiyo ODM, twende uchaguzi, Raila awe rais, Musalia awe naibu rais na mimi niwe waziri mkuu. Sasa kufika kwa uchaguzi, mambo yakabadilika, tukakosa kiti ya rais, naibu rais. Kilichopatikana ni kiti cha Waziri Mkuu.”
Ruto aliendelea kuonyesha kuwa aligeukwa na wenzake kwa sababu alitarajia labda angepewa fursa ya kuwa naibu Waziri mkuu wala sio waziri.
Nafasi hizo zilipatikana baada ya makubaliano ya serikali ya Muungano kati ya ODM na muungano wa PNU ulioongozwa na Mwai Kibaki.
Hata hivyo mwenyekiti wa ODM wakati huo John Mbadi alisema kuwa walikubaliana kuwa nafasi ya pili waliopewa ambayo ni kubwa ipewe Musalia Mudavadi.
Ilivyojitokeza ni kana kwamba Ruto alihisi kusalitiwa hasa kwa kuona kuwa alichangia pakubwa kwenye uchaguzi wa mwaka 2007 ikilinganishwa na Mudavadi.
Lakini uhusiano wa Raila na Odinga ulibadilika kabisa kiasi cha kutoweza kurekebishwa baada ya Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ya ICC, ilipoingilia ghasia za uchaguzi za 2007.
Pia akiwa Waziri Mkuu, Raila Odinga aliunga mkono kuondolewa kwa watu katika Msitu wa Mau ambao wengi wao walitoka jamii ya Kalenjin ambayo ni ya Ruto anayedai kuwa walichangia pakubwa katika kumpigia kura mwaka 2007.
Wafuasi wa Ruto walidai kuwa Odinga amewasaliti, aliwanyanganya kiti, sasa anawapokonya mashamba na suala hilo likafanyiwa siasa kweli.
“Hadi leo, bado ninafurahia nilichokifanya (katika msitu wa Mau) hatua ya utunzaji na faida zake kwa watu wetu. Wale wanaoamini kwa wakati wa sasa na wanaojifaidi wenyewe hawatafanya kazi ya uhifadhi…”, Raila alisema wakati akipokea tuzo kwa uhifadhi wa mazingira.
Wakati mwendesha mashitaka wa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Jinai (ICC) Luis Moreno Ocampo alipotoa orodha ya washukiwa. Raila Odinga awali alionekana kumtetea Ruto kwa kusema alikuwa mwathirika na sio mtekelezaji wa ghasia hizo lakini baadaye akaonekana kuunga mkono kesi za ICC dhidi ya Ruto na Uhuru Kenyatta.
Wachambuzi wakati huo walisema labda pengine hilo lilitokana na dhana kuwa wakiwa wawili hao hawapo kwenye uchaguzi wa 2013, basi huenda mambo kwake yakawa mteremko.
Lakini kama fikra zilikuwa hizo, basi hesabu ziliteleza mahali kwani ICC ilikuwa mwanzo wa muungano wa Uhuru Kenyatta na William Ruto.
Na ilipofika uchaguzi 2013, walishinda kwa kishindo, Raila akaishia kuambulia patupu.
Na mwaka 2017 Uhuru Kenyatta na William Ruto wakashinda tena kwenye uchaguzi lakini ushindi wao ulifutiliwa mbali na mahakama ya Juu kabisa baada ya Raila Odinga kupinga matokeo yake. Jaji Mkuu wa Kenya wakati huo David Maraga alisema uchaguzi huo ulikumbwa na dosari myingi na kuagiza mchakati huo urudiwe tena. Raila Odinga alisusia uchaguzi wa marudio na kujiapisha kama “Rais wa Watu”.
Lakini kama pengine ulidhani huo ndio ulikuwa mwisho wa Raila umekosea, kitendo cha Raila kupeana mkono na Rais Uhuru Kenyatta mnamo Machi 9, 2018 kilishangaza taifa. Lakini kusalimiana kwa mikono au ‘Handshake’ kulimaliza machafuko ya miezi kadhaa na kupelekea Mpango wa Building Bridges Initiative (BBI), ajenda ya mageuzi ya katiba iliyolenga kushughulikia dosari za kihistoria na kukabiliana na ukosefu wa haki.
Ingawa Raila alikanusha kunufaika binafsi, wengi wa wafuasi wake walihisi makubaliano hayo yalipunguza sauti ya upinzani.
BBI hiyo ikawa tena, mgawanyiko wa Raila na Ruto ambaye alipinga BBI.
William Ruto alikosoa mpango huo na kutaja makubaliano hayo kuchanganyikiwa. Ruto alisema kuwa Handshake ”ilikuwa na utapeli na ukora mwingi”.
Baadaye BBI ilifutiliwa mbali na mahakama, na azma ya Raila ya urais 2022 – akiungwa mkono na Uhuru Kenyatta – ilimalizika kwa kushindwa na William Ruto.
Hakuna uadui wa kudumu katika siasa
Lakini kama ulifikiria uhasama wa kisiasa ni wa kudumu, tafakari tena hilo. Hata baada ya kufanyiana vitimbi, kuitana majina na kila aina ya vituko, Mwaka huu wa 2025, Raila Odinga na Rais William Ruto waliketi kwenye meza ya mazungumzo na kufikia makubaliano ya kisiasa. Hii ilifanyika baada ya maandamano Juni 2024 yaliyoongozwa na vijana maarufu Gen Z.
Ndoa ya kisiasa ikabuniwa kati ya Raila Odinga na Rais William Ruto.
Hata hivyo, hatua hiyo haikupokelewa kwa moyo mkunjufu na wote.
“Huu ni usaliti kwa Wakenya,” alisema kiongozi wa chama cha Wiper Democratic Movement Kalonzo Musyoka ambaye amewahi kuwa mgombea mwenza wa Odinga katika chaguzi mbili (2013 na 2017), na pia alikuwa makamu wa rais wa Kenya (2008-2013).
Hata hivyo, makubaliano hayo yalionekana kumtenga Naibu wa Rais wa William Ruto, Rigathi Gachagua ambaye baadaye aliondolewa uongozini.
Na ikiwa sio mara ya kwanza, Raila alivyojipata ndani ya serikali kati yake na Uhuru Kenyatta, ndivyo alivyojipata tena ndani ya serikali ya Ruto.
Mwaka 2024, Raila alitangaza kuwania mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika hatua iliyoungwa mkono kwa asilimia 100 na Ruto. Na muda mfupi baadaye, Ruto alichukua hatua na kuanza kuzunguka kila pembe ya Afrika kumfanyia Raila kampeni. Ingawa kiti hicho kiliwaponyoka, walitembea pamoja hadi dakika ya mwisho.
Wakati huu, wakionekana kuwa maswaiba na hadi kifo chake, unaweza kusema walikuwa marafiki wa kufa kuzikana.
Ruto amethibitisha hilo kwa kumpa Raila Odinga mazishi ya serikali jambo ambalo hata baba yake Raila Odinga, Jaramogi Oginga Odinda hakufanyiwa licha ya kuwa naibu rais wa kwanza wa Kenya.