
Serikali ya Kenya imetangaza kuwa Siku ya Mashujaa itaadhimishwa leo kama kawaida licha ya hofu iliyokuwepo kwamba ingeahirishwa baada ya kifo cha waziri mkuu wa zamani wa nchi hiyo, Raila Odinga.
Msemaji wa Serikali ya Kenya, Isaac Mwaura amesema: “Ni vizuri kutambua kuwa siku hii ya Mashujaa itatumika kuwatambua mashujaa wetu, na Raila atakuwa kati ya wale ambao watatambuliwa na kuenziwa”
Bwana Mwaura amesema, Serikali inatoa wito kwa Wakenya wa matabaka mbalimbali wajitokeze kwa maadhimisho ya Mashujaa kama sehemu ya kuendelea kumuezi Raila Odinga.
Sikukuu ya Mashujaa huandaliwa kila mwaka nchini Kenya kuwakumbuka mashujaa waliopigania uhuru wa taifa hilo.
Amesema hayo akikanusha habari zilizoenea mitandaoni kuwa sherehe hiyo ingeahirishwa kutokana na mauti na mazishi ya Raila.
Bw Odinga alizikwa Kang’o Ka Jaramogi, kando ya kaburi la baba yake na karibu na wanafamilia katika hafla iliyoongozwa na Rais William Ruto na viongozi wengine wa ndani na nje ya nchi.