Mgonjwa wa mwisho wa Ebola aliyelazwa katika kituo cha matibabu cha Bulape katika Mkoa wa Kasai, nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, ametangazwa kuwa amepona na kuruhusiwa kuondoka kituoni hapo siku ya Jumapili, Oktoba 19, 2025. Kuruhusiwa kuondoka kwa mtu huyo kutafuatiwa na siku 42, baada ya hapo janga hilo linaweza kutangazwa rasmi kuwa limeisha, mradi tu hakuna kesi mpya itakayogunduliwa katika kipindi hiki, kulingana na Shirika la Afya Duniani WHO.

Imechapishwa:

Dakika 1 Wakati wa kusoma

Matangazo ya kibiashara

Tangu janga hilo lilipotangazwa mnamo Septemba 4, 2025, wagonjwa 64 walirekodiwa, ikiwa ni pamoja na 53 waliothibitishwa na 11 walioshukiwa kuamukizwa virusi vya ugonjwa huo. Kufikia sasa, wagonjwa 19 wamepona, na hakuna kesi mpya iliyoripotiwa tangu Septemba 25.

Licha ya changamoto za vifaa kuhusiana na hali ya maeneo ya vijijini na barabara, Wizara ya Afya ya DRC, kwa usaidizi mkubwa wa WHO na washirika wake, imeongeza hatua za kukabiliana na ugonjwa huo, kupeleka timu za wataalamu mbalimbali kwa ajili ya ufuatiliaji, huduma za kliniki, kuzuia na kuhamasisha jamii.

Kituo cha matibabu ya Ebola chenye vitanda 32, kikiwemo chumba cha wagonjwa mahututi, kiliwekwa haraka huko Bulape. Zaidi ya watu 35,000 wamechanjwa dhidi ya virusi hivyo katika eneo hili. Hatua hii muhimu inawakilisha maendeleo makubwa katika mapambano dhidi ya janga hili, lakini umakini unabaki kuwa muhimu ili kuzuia kutokea tena kwa virusi hivi.

Dkt. Mohamed Janabi, Mkurugenzi wa WHO kanda ya Afrika, amepongeza juhudi zilizofanywa katika mapambano dhidi ya janga hilo, akisema: “Kupona kwa mgonjwa wa mwisho, wiki sita tu baada ya kutangazwa kwa mlipuko huo, ni mafanikio ya ajabu. Inadhihirisha nguvu ya ushirikiano, utaalamu wa kitaifa, na azimio la pamoja la kushinda vikwazo ili kuokoa maisha ya watu.” 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *