Trump aliitoa kauli hiyo wakati alipokutana kwa mazungumzo na Zelensky akipendekeza uwepo wa mpango wa usitishwaji mapigano katika maeneo ya mstari wa mbele wa vita na kumtaka Zelensky kukubali kuyaachia maeneo yaliyonyakuliwa na Urusi, wazo linalopingwa vikali na Zelensky.

Vyanzo kadhaa vimesema Trump huenda alishawishiwa na Putin wakati walipozungumza kwa njia ya simu siku ya Alhamisi ambapo kulingana na gazeti la “The Washington Post”, Putin alipendekeza  Ukraine  kuiachia mikoa ya Donetsk na Luhansk na kusalia sehemu ndogo ya Zaporizhzhia na Kherson. Trump alitangaza pia kusitisha azma ya kuipatia Ukraine makombora ya masafa marefu ya Tomahawks akisema kuwa nchi yake pia inayahitaji:

Marekani I Rais Donald Trump akizungumza na rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky
Rais wa Marekani Donald Trump (kulia) akizungumza na mwenzake wa Ukraine Volodymyr ZelenskyPicha: Evan Vucci/AP Photo/picture alliance

” Ni silaha kubwa na hatari, lakini tunapaswa kukumbuka jambo moja,  sisi wenyewe tunazihitaji pia. Unajua, hatuwezi kuipatia Ukraine silaha zetu zote, ni jambo lisilowezekana. Nimekuwa mwema kwa Ukraine na Rais Zelensky lakini kwa hilo hatuwezi, sitaki tupungukiwe silaha hizo na siwezi kuiweka Marekani hatarini.”

Aidha Trump, amesema atasimamia makubaliano hayo kwa kutoa hakikisho la usalama kwa pande zote, kauli iliyowachukiza maafisa wa Ukraine waliohudhuria mkutano huo wa Ijumaa.

Kwa upande wake Zelensky amemuomba  Trump  kumshinikiza zaidi Putin kumaliza vita akisisitiza kuwa Urusi ina nguvu kuliko kundi la Hamas, hivyo itakuwa vigumu kufikia makubaliano ya amani huku rais huyo wa Marekani akimsisitizia Zelensky kwamba Putin ametishia “kuiharibu” Ukraine ikiwa haitatii masharti hayo.

Urusi na Ukraine zashambuliana usiku kucha

Pawlohrad 2025 | Vikosi vya Ukraine vikijaribu kudungua droni
Vikosi vya Ukraine vikijaribu kudungua droni zilizorushwa na UrusiPicha: Roman Pilpey/AFP

Hayo yakiarifiwa, Urusi na Ukraine zimeshambuliana kwa makombora na droni usiku kucha. Moscow imetangaza kuwa watu wawili wameuawa katika eneo lake la Belgorod.

Ukraine ilishambulia pia kiwanda cha kusindika gesi kusini mwa Urusi, na kupelekea kusimamishwa kwa shughuli za kusafirisha gesi kutoka Urusi kuelekea Kazakhstan.

Kwa upande wake Urusi nayo ilifanya  mashambulizi  makubwa na kuulenga mgodi wa makaa ya mawe katika mkoa wa Ukraine wa Dnipropetrovsk. Ukraine pia imesema ilidungua droni zaidi ya 50 zilizorushwa na Urusi usiku kucha.

Katika hatua nyingine, mawaziri wa mambo ya nje wa Umoja wa Ulaya wanatarajiwa kukutana siku ya Jumatatu huko Luxembourg kujadili mzozo wa Ukraine na ule wa Mashariki ya Kati.

// AFP, AP, RTR, DPA

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *