
NAIROBI – Shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu, Amnesty International, limeeleza wasiwasi wake kuhusu kile linachotaja kuwa “wimbi la hofu na ukandamizaji” nchini Tanzania, wiki chache kabla ya uchaguzi mkuu wa tarehe 29 Oktoba 2025.
Imechapishwa:
Dakika 2 Wakati wa kusoma
Matangazo ya kibiashara
Katika ripoti yake mpya iliyopewa jina “Bila Kupingwa, Bila Kukosolewa, Bila Haki”, Amnesty inasema serikali imeendeleza mkakati wa makusudi wa kuzuia ushiriki wa raia na kudhibiti maoni yanayopinga serikali, kupitia kuwakamata raia kiholela na kufungia wapinzani muhimu wa kisiasa.
“Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan imekatisha matumaini ya mageuzi. Badala yake, imeendeleza vitendo vya ukandamizaji vinavyolenga wapinzani, wanahabari na asasi za kiraia,” alisema Tigere Chagutah, Mkurugenzi wa Amnesty International Kanda ya Afrika Mashariki na Kusini mwa Afrika.
Ripoti hiyo inaeleza kwamba wagombea wawili wakuu wa upinzani, akiwemo Tundu Lissu wa Chadema, wamezuiwa au kukabiliwa na mashtaka yaliyochochewa kisiasa. Lissu bado anashikiliwa kwa kosa la uhaini kutokana na maoni aliyotoa mitandaoni mwezi Aprili 2025.
Amnesty pia imeeleza kuwa mfumo wa sheria umetumika “kama silaha” dhidi ya wapinzani, huku baadhi wakiteswa, kupotezwa au kuuawa. Mfano ni kisa cha Ali Mohammed Kibao, mwanachama wa chama cha upinzani cha Chadema, aliyepatikana amekufa baada ya kutekwa jijini Dar es Salaam, na wengine kadhaa ambao hawajulikani walipo hadi sasa.
Kwa mujibu wa Amnesty, Chama cha Wanasheria wa Tanganyika kimeripoti zaidi ya visa 80 vya watu waliopotea katika mazingira ya kutatanisha tangu Agosti 2024.
“Serikali lazima isitishe mara moja kampeni yake ya ukandamizaji na iondoe mashtaka yote yanayochochewa na siasa,”
amesema Chagutah.
Shirika hilo limekosoa pia matumizi ya sheria mpya za mwaka 2024 kuhusu yyama vya siasa na tume huru ya taifa ya uchaguzi, likidai zinadhoofisha uhuru wa wananchi kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Aidha, limeorodhesha matukio kadhaa ya kuvuruga mikutano ya amani, kuwakamata viongozi wa upinzani kama Amani Golugwa, na kuzuia uhuru wa kujieleza, hasa kupitia mitandao ya kijamii.
“Bila shinikizo endelevu kutoka kwa jamii ya kimataifa, uchaguzi wa 2025 unaweza kuwa wa kiutaratibu tu bila uhalali,”
ameonya Chagutah.
Mnamo Machi 2021, Samia Suluhu Hassan aliapishwa kuwa rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania kufuatia kifo cha John Magufuli. Awali, aliahidi mageuzi ya kisiasa na uhuru wa vyombo vya habari, lakini Amnesty inasema matumaini hayo “yamefifia” huku ukandamizaji ukiongezeka kuelekea uchaguzi.
Ripoti ya mwaka 2020 ya shirika hilo pia ilikuwa imetoa tahadhari kuhusu “matumizi ya sheria kama silaha” dhidi ya wapinzani na wanaharakati nchini humo.