Hujambo msikilizaji mpenzi, nina wingi wa matumaini kwamba u mzima wa afya. Karibu tuangazie japo kwa ufupi, baadhi ya matukio makubwa yaliyojiri viwanjani katika muda wa siku zilizopita, kitaifa, kieneo na kimataifa. Nakusihi usibanduke hapo ulipo hadi tamati ya kipindi….
Ali Akbar Gharibshahi, bingwa wa mchezo wa kunyanyua vitu vizito wa Iran ameweka rekodi mpya ya dunia na kushinda medali ya dhahabu katika kategoria ya kilo wanamichezo wenye 107, kwenye Mashindano ya Dunia ya Kunyanyua Uzani ya 2025 nchini Misri. Gharibshahi aliibuka kidedea kwa kunyanyua uzani wa kilo 255, na kuboresha rekodi yake mwenyewe ya dunia aliyoweka katika Michezo ya Walemavu ya 2024 huko Paris, aliponyanyua kilo 252. Ingawaje alishindwa kunyanyua kilo 260 kwenye jaribio lake la mwisho, lakini umbuji wake kwenye raundi ya pili ulitosha kumpa medali ya dhahabu na kuweka rekodi mpya ya dunia.

Wanamichezo kutoka mataifa 70 wanapambana kufa kupona kusaka medali tofauti, huku Misri ikiwa mwenyeji wa duru hiyo ya kwanza ya Mashindano ya Dunia ya Kunyanyua Uzani ya Walemavu (Para Powerlifting World). Roohollah Rostami wa Iran (wanaume wasiozidi kilo 88), Amir Jafari (wanaume wenye kilo 72) na Mohsen Bakhtiar (wanaume wenye kilo 65) awali walikuwa wameshinda medali tatu za fedha katika mashindano hayo ya kimataifa. Aidha Ahmad Aminzadeh wa Iran alitwaa medali ya dhahabu katika mashindano hayo siku ya Ijumaa. Alishika nafasi ya kwanza akiwa na kilo 260 katika +107kg ya wanaume. Kadhalika Aliakbar Gharibshahimen katika kilo 107 alikuwa ameshinda medali ya dhahabu. Roohollah Rostami (wanaume hadi kilo 88), Amir Jafari (wanaume hadi kilo 72) na Mohsen Bakhtiar (wanaume hadi kilo 65) pia walikuwa wameshinda medali tatu za fedha katika mashindano hayo. Msururu endelevu wa Iran wa kuvunja rekodi na kuvuna medali lukuki umeifanya kuwa moja ya mataifa yenye mafanikio zaidi katika historia ya mchezo wa kuinua vyuma vizito. Ushindi huo unaongeza idadi ya medali za Iran na kupiga jeki kasi ya timu hiyo ya Jamhuri ya Kiislamu, kabla ya maandalizi ya Michezo ya Walemavu ya 2028.
Upigaji Makasia; Mabanati wa Iran wang’ara Vietnam
Fatemeh Mojallal wa Iran alishinda medali ya dhahabu katika Mashindano ya Kupiga ya Makasia ya 2025 siku ya Jumapili. Mojallal alivuka mstari wa kumaliza katika uzito wa juu wa single ya wanawake wa sculls kwa muda wa 8:31.11 na kushinda medali ya dhahabu. Aidha Zeynab Norouzi alishinda medali ya fedha katika uzani mwepesi wa single ya wanawake kwa muda wa 8:24.75. Mpiga makasia wa Hong Kong alitwaa dhahabu, huku medali ya shaba ikienda kwa mpanda makasia kutoka Kazakhstan. Iran tayari ilikuwa imeshinda medali moja ya dhahabu na mbili za shaba katika siku ya kwanza ya mashindano hayo.

Wanariadha wa kike wa Iran walijishindia medali ya dhahabu katika uzani mwepesi wa kupiga makasia katika Mashindano ya Mashindano ya Makasia ya Asia nchini Vietnam. Wawili hao wa Zeinab Norouzi na Kimia Zarei walichuana na timu kutoka India, Vietnam, Thailand, na Hong Kong katika fainali. Wanaspoti hao wa Kiirani walimaliza wa kwanza kwa muda wa 7:30.22, na kupata medali ya dhahabu. Mashindano hayo yalianza Oktoba 17 katika Kituo cha Mafunzo ya Makasia cha Hai Phong, huko Hai Phong, Vietnam.
Ligi ya Mabingwa Afrika; Simba yanguruma
Wekundu wa Msimbazi, Simba SC, wamejiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini FC ya Eswatini, katika mchezo wa mkondo wa kwanza wa hatua ya pili ya michuano hiyo, uliochezwa leo Oktoba 19, 2025. Mabao ya Simba yalifungwa na Wilson Nnang’u dakika ya 45+2 kipindi cha kwanza, kabla ya Kibu Denis kuhitimisha ushindi huo kwa mabao mawili dakika ya 85 na 90+1. Ushindi huo unaiweka Simba SC kwenye nafasi nzuri kuelekea mchezo wa marudiano utakaochezwa wiki ijayo katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam. Mshindi wa jumla wa michezo hiyo miwili atasonga mbele kuingia hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Nayo klabu ya Azam ya Tanzania imejiweka pazuri kutinga hatua ya makundi, baada ya kuichakaza KMKM mabao 2-0 wikendi katika Uwanja wa New Amaan Complex visiwani Zanzibar. Azam inapambana kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza. Mabao yake kwenye mchuano huo wa ugenini yalifungwa na Jephte Kitambala Bola na Pascal Msindo.
Katika Uwanja wa Intwari huko Bujumbura, mji mkuu wa Burundi, Singida Black Stars ya Tanzania iliwalazimisha wenyeji Flambeau du Centre sare ya bao 1-1. Bao la Singida kwenye mchezo huo wa ugenini lilifungwa na Clatous Chama. Singida sasa watahitaji sare tasa au ushindi wa aina yoyote Jumapili ijayo ili waweza kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika. Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga SC, wamekubali kichapo cha bao 1-0 kutoka kwa Silver Strikers katika mchezo wa hatua ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Jumamosi ya Oktoba 18, 2025, nchini Malawi. Yanga SC sasa inalazimika kushinda katika mchezo wa marudiano jijini Dar es Salaam ili kufufua matumaini ya kusonga mbele kwenye michuano hiyo mikubwa barani Afrika.
Kwa upande wake, klabu ya Nairobi United ya Kenya iliichabanga Etoile Sportive du Sahel ya Tunisia mabao 2-0 katika Uwanja wa Ulinzi Sports Complex jijini Nairobi Jumapili. Pamoja na miamba hao wa Tunisia kumchezesha beki wa zamani wa Kariobangi Sharks na Gor Mahia Alphonce Omija katika kikosi chao, lakini walishindwa kuzuia makombora ya United, achilia mbali wao kuona lango la mahasimu. Kwa ushindi huo, United imepiga hatua kubwa kuelekea hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho. Wametangaza kutunuku ushindi wao kwa aliyekuwa Waziri Mkuu wa Kenya, Raila Odinga aliyefariki dunia Jumatano iliiyopita.
Ulimwengu wa Michezo wamuomboleza Odinga
Ulimwengu wa michezo nchini Kenya unaomboleza kifo cha mmoja wa mashabiki wakubwa wa michezo nchini humo, Raila Amolo Odinga mnamo Jumatano, Oktoba 15, 2025. Kiongozi huyo mashuhuri anayejulikana kwa majina kama Tinga, Baba, RAO, na Agwambo, alikuwa shabiki mkubwa wa Gor Mahia, Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza na pia timu ya taifa ya Kenya, Harambee Stars. Odinga aliaga dunia nchini India alipokuwa akipokea matibabu. Ripoti kutoka India zinasema alizimia wakati wa matembezi ya asubuhi na kufariki. Shirikisho la Soka Kenya (FKF) limesema linaungana na taifa kuomboleza kifo cha Mheshimiwa Odinga. “Alikuwa kiongozi mwenye maono na shabiki wa kweli wa kandanda ya humu nchini. Urithi wake utaendelea kuhamasisha vizazi vijavyo. Tunatuma rambirambi zetu kwa familia yake, marafiki, na Wakenya wote katika wakati huu mgumu,” FKF inayoongozwa na Hussein Mohammed, ilisema.

Shirikisho la Raga la Kenya (KRU) pia limesema: “Jumuiya ya raga inaungana na taifa kuomboleza kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga. Tunatuma salamu za pole kwa familia yake na Wakenya wote. Mchango wake katika kuijenga Kenya yenye umoja na maendeleo unabaki kuwa mwanga kwetu sote. Kama jamii ya raga, tunaheshimu urithi wake wa uongozi na uzalendo.” Klabu ya Gor Mahia, ambayo Odinga alikuwa mlezi wake kwa miaka 20, imemuomboleza ikisema: “Mioyo yetu imejaa huzuni kufuatia kifo cha mlezi wetu mpendwa, Mheshimiwa Raila Odinga. Alikuwa nguzo na mwanga kwa klabu yetu. Tunatuma rambirambi kwa familia yake. Pumzika kwa amani Baba.” Waziri wa Michezo, Salim Mvurya, amesema taifa limepoteza nguzo kubwa ya uongozi. “Raila alikuwa mtu mwenye ujasiri, maono, na imani isiyotetereka katika demokrasia ya Kenya. Natoa rambirambi zangu kwa Mama Ida Odinga, familia ya Odinga, marafiki, na Wakenya wote. Raila alikuwa mwalimu kwa wengi, akiwemo mimi, na alijitolea kupigania ugatuzi, usawa, na taifa lenye umoja. Urithi wake wa uvumilivu, kujitolea na uzalendo utaendelea kuongoza safari ya kidemokrasia ya Kenya.” Hali kadhalika, Televisheni ya Mashabiki wa Arsenal (AFTV) imemuomboleza Odinga kwa njia ya kipekee, katika ujumbe wa kugusa moyo uliosambazwa kwenye mitandao yake ya kijamii. AFTV ndiyo chaneli kubwa zaidi ya mashabiki duniani, ambayo huwashirikisha mashabiki wa Arsenal inayoshiriki Ligi Kuu ya Uingereza.
Dondoo za Hapa na Pale
Waziri wa Michezo na Vijana wa Iran, Ahmad Donyamali, amemtaka mwenzake wa Uhispania, Pilar Alegria, kutekeleza jukumu lake kuu la kuunda makubaliano ya kimataifa ya kuusimamisha utawala wa Israel katika michezo ya kimataifa. Katika barua yake kwa Alegria siku ya Jumatano, Donyamali alitoa alipongeza nafasi ya Uhispania ya kulaani mauaji ya halaiki yanayofanywa na utawala wa Kizayuni huko Gaza. Amemsihi Waziri wa Elimu, Mafunzo ya Ufundi na Michezo wa Uhispania kuongoza juhudi katika kujenga maelewano ya kimataifa ya kuzuiwa utawala wa Kizayuni kushiriki katika mashindano yoyote duniani.
Mbali na hayo, Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) limemteua Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Wallace Karia, kuwa Makamu wa Rais wa Kamati ya Soka la Ufukweni ya FIFA kwa kipindi cha miaka minne, hadi mwaka 2029. Aidha Rais wa Klabu ya Yanga SC, Eng. Hersi Said, ameteuliwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kuwa Mjumbe wa Kamati ya Mashindano ya Vilabu vya Wanaume Duniani kwa kipindi cha miaka minne, kuanzia mwaka 2025 hadi 2029.
Mbali na hayo, historia iliwekwa kwenye Tuzo za AFC Riyadh 2025 siku ya Alhamisi huku Marziyeh Jafari akiwa mshindi wa kwanza kabisa wa AFC wa Mwaka (Wanawake) kutoka Iran. Jafari ambaye ni mtu mashuhuri katika mazingira ya ukufunzi wa Asia, alitunukiwa kwa kuiongoza Iran kwa mafanikio katika kufuzu kwa Kombe la Asia la Wanawake la AFC Australia 2026, na kufanikiwa kucheza mara ya pili mfululizo kwenye maonyesho ya Bara baada ya mechi yao ya kwanza mwaka wa 2022. Huku wakihitaji ushindi katika mchuano wao wa mwisho wa Hatua ya Kundi dhidi ya Jordan, Jafari alipanga ushindi muhimu wa 2-1 ili kutinga hatua ya kufuzu—jambo ambalo lilistaajabisha zaidi kwa kuwa alikuwa amechukua jukumu takriban miezi mitatu iliyopita. Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 43, mteule wa tatu pekee kutoka Iran baada ya Shahrzad Mozafar (2010) na Katayoun Khosrowyar (2019), sasa ndiye mshindi wa 15 wa tuzo hii, ambayo pia ilitambua mafanikio yake katika ngazi ya klabu akiwa na Bam Khatoon Women’s FC.
Kwengineko, mwandakandanda nguli wa klabu ya Paris Saint-Germain ya Ufaransa, Ousmane Dembele, ameiomba timu yake kumpa mkataba mpya na ongezeko la mshahara linalolingana na hadhi yake mpya kama mshindi wa Ballon d’Or 2025. Kwa sasa Dembele analipwa takribani euro milioni 18 kwa mwaka na bado ana mkataba unaomfunga na PSG hadi mwaka 2028. Hata hivyo, baada ya mafanikio yake binafsi na ushindi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya, winga huyo wa Ufaransa anahisi ni wakati wa kutambuliwa kifedha.
Taarifa kutoka L’Équipe zinaeleza kuwa mkataba wa Dembele unaweza kuwa na kipengele cha nyongeza ya mshahara endapo atashinda Ballon d’Or jambo ambalo PSG inakanusha rasmi. Hata hivyo, wawakilishi wa Dembele wanataka klabu iheshimu kipengele hicho, wakisema mafanikio yake ni ishara tosha ya kuthibitisha ubora wake duniani.
Na mshambuliaji nyota wa Ureno na klabu ya Al-Nassr, Cristiano Ronaldo, ametajwa kuwa mchezaji wa kwanza wa soka kufikia hadhi ya bilionea, kwa mujibu wa ripoti mpya ya chombo cha masuala ya fedha, Bloomberg. Ripoti ya “Bloomberg Billionaires Index”, inayofuatilia watu matajiri zaidi duniani kulingana na thamani yao halisi, imemkadiria Ronaldo kuwa na utajiri unaofikia dola bilioni 1.4 za Marekani (£1.04bn). Kwa mujibu wa Bloomberg, tathmini hiyo inajumuisha mapato yake ya uwanjani, uwekezaji na mikataba ya matangazo.

Imebainika kuwa Ronaldo alipata zaidi ya dola milioni 550 (£410m) kama mishahara kati ya mwaka 2002 hadi 2023, huku sehemu kubwa ya mapato yake ikitokana na mikataba ya udhamini, ikiwemo ule wa muda mrefu na Nike unaokadiriwa kufikia dola milioni 18 (£13.4m) kwa mwaka. Ronaldo alipojiunga na Al-Nassr ya Saudi Arabia mwaka 2022, alitajwa kuwa mchezaji anayelipwa zaidi katika historia ya soka, akipokea mshahara wa takriban pauni milioni 177 kwa mwaka.
…………………MWISHO….…………