
Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran (IRGC) limesema kuwa limejiandaa kikamilifu kukuza ushirikiano wa kimkakati na vikosi vya ulinzi vya Yemen katika mapambano dhidi ya mabeberu wa dunia na Uzayuni wa kimataifa.
Kamanda Mkuu wa IRGC, Meja Jenerali Mohammad Pakpour, jana aliwasilisha salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Majeshi ya Yemen, Brigedia Jenerali Youssef Hassan Al-Madani kufuatia kuuawa shahidi Meja Jenerali Mohammad Abdul Karim al-Ghamari, ambaye alifariki dunia kutokana na majeraha aliyopata katika mashambulizi ya anga ya Israel.
Meja Jenerali al Ghamari aliuliwa akiwa pamoja na wenzake kadhaa na mtoto wake wa kiume aliyekuwa na umri wa miaka 13 kwa jina la Hussein.
Kamanda Mkuu wa IRGC amesema kuwa kifo cha Ghamari kitazidisha azma ya kishujaa ya taifa la Yemen ya kupambana na maadui wa nchi za Kiislamu katika kuwapigania watu waliokandamizwa na wanaopigania haki duniani hususan watu madhulumu wa Ukanda wa Gaza huko Palestina.
Meja Jenerali Mohammad Pakpour pia amempongeza Brigedia Jenerali Youssef Hassan Al-Madani kwa kuteuliwa kuwa Mkuu wa Majeshi ya Yemen. Amesema uteuzi huo unaashiria wazi kuendelezwa njia ya Ghamar na kuimarishwa safu ya mapambano dhidi ya maadui.