Shirika la Afya Duniani (WHO) jana liliripoti kuwa mgonjwa wa mwisho wa Ebola aliruhusiwa jana kutoka kwenye kituo cha matibabu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Katika video iliyotumwa kwenye mitandao ya kijamii, wafanyakazi wa sekta ya tiba wameonekana wakisherehekea baada ya mgonjwa wa mwisho wa Ebola kuruhusiwa kurudi nyumbani. 

WHO imesema katika taarifa yake kuwa hiyo ni hatua muhimu kuelekea kuhitimisha mripuko wa ugonjwa wa Ebola huko Kongo. Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tayari imeanza kuhesabu siku 42 kuweka wazi kuwa mripuko wa ugonjwa wa Ebola umemalizika iwapo hazitathibitishwa kesi mpya za homa hiyo. 

Profesa Mohamed Janabi, Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani katika Kanda ya Afrika, amesema kuwa kupona kwa mgonjwa wa mwisho wiki sita tu baada ya  kutangazwa mripuko huo ni mafanikio ya kushangaza ambayo yanaonyesha namna ushirikiano imara, weledi wa taifa na jitihada zilivyochangia kushinda changamoto za kuokoa na kulinda maisha ya wananchi. 

WHO imesema kuwa wagonjwa 19 wamepona ugonjwa wa Ebola ambapo tangu Septemba 25 hadi sasa hakuna kesi mpya za ugonjwa huo zilizoripotiwa. Watu 53 walithibitishwa kuugua Ebola nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu kuripotiwa mripuko wa ugonjwa huo nchini humo. 

Itakumbukwa kuwa, mripuko wa karibuni wa ugonjwa wa Ebola uliripotiwa na mamlaka husika za Kongo tarehe 4 Septemba mwaka huu katika ukanda wa afya wa Bulape katika jimbo la Kasai linalopakana na Angola. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *