
Idara ya Vyombo vya Habari ya Serikali katika Ukanda wa Gaza imesema ukiukaji wa Israeli wa mapatano ya kusitisha vita unaakisi hamu ya utawaka huo vamizi ya kuzidisha machafuko na mtazamo wake wa kichokozi dhidi ya watu wa ukanda huo.
Idara hiyo imetangaza kuwa vikosi vya utawala ghasibu wa Israel vimefanya msururu wa ukiukaji mkubwa na wa mara kwa mara tangu baada ya makubaliano ya kusitisha mapigano. Imesema kufikia jana Jumapili, idadi ya ukiukaji huo wa mapatano ya kusitisha vita ilifikia 80, katika ukiukaji wa wazi wa azimio la kusitisha mapigano na sheria ya kimataifa ya kibinadamu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa ukiukwaji huo ni pamoja na kuwafyatulia risasi raia moja kwa moja, mashambulizi ya makusudi ya mabomu, kutumia mikanda ya moto na kukamatwa raia.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa vikosi vya utawala vamizi wa Israel vimetekeleza mashambulizi hayo kwa kutumia vifaru na magari ya kivita yaliyowekwa pembezoni mwa vitongoji vya makazi ya raia, vifaa vya kielektroniki vyenye sensa na vya kulenga mbali, na ndege za kivita na quadcopter ambazo zinaendelea kupaa juu ya maeneo ya makazi ya watu na kuwafyatulia risasi raia moja kwa moja.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mashambulizi hayo yamesababisha vifo vya Wapalestina 97 na wengine zaidi ya 230 kujeruhiwa tangu kusainiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano. Taarifa hiyo imeonya kuwa kuendelea ukiukaji huo kunatishia kusambaratika kabisa makubaliano ya kusitisha mapigano.